Msemaji wa M23, Willy Ngoma, auawa katika shambulio la droni mashariki mwa DRC

Msemaji wa kundi la waasi la M23 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Willy Ngoma, ameuawa katika shambulizi la ndege zisizo na rubani mashariki mwa DRC siku ya Jumanne.

By
Msemaji wa kundi la waasi la M23 nchini DRC, Willy Ngoma, ameuawa katika shambulizi la ndege zisizo na rubani mashariki mwa DRC. / / Reuters

Reuters imemnukuu mwanadiplomasia wa eneo hilo, afisa mmoja mwandamizi wa kundi hilo na mshauri wa serikali ya nchi za Magharibi akithibitisha kifo chake.

M23 inadhibiti maeneo makubwa ya majimbo ya Kivu Kaskazini na Kusini baada ya mashambulizi ya mwaka 2025 ambapo waasi hao waliteka miji ya kimkakati ya Goma na Bukavu.

Mauaji hayo yametokea wakati juhudi za kusitisha mapigano zinazosimamiwa na Qatar zikiendelea, huku serikali ya DRC na M23 zikiwa zimesaini makubaliano jijni Doha ya kuanzisha utaratibu wa pamoja wa kufuatilia na kuthibitisha usitishaji vita, ukiwahusisha Qatar, Marekani na Umoja wa Afrika kama waangalizi.

Shambulio hilo lilitokea karibu na eneo la Rubaya, katika mkoa wa Kivu Kaskazini, majira ya saa tisa usiku (0100 GMT), na lilifuata siku kadhaa za mashambulizi ya mara kwa mara ya ndege zisizo na rubani katika eneo hilo, yaliyotekelezwa na jeshi la Congo, afisa huyo mwandamizi wa M23 aliiambia Reuters.

Rubaya ni kitovu muhimu cha uchimbaji wa madini ya coltan kinachozalisha takribani asilimia 15 ya usambazaji wa madini hayo duniani, jambo linalofanya kuwa ngome muhimu ya kifedha kwa waasi wa M23.