| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Kenya yapata Askofu Mkuu mpya huku Papa akipandisha hadhi Jimbo Kuu la Eldoret
Hatua hii inafanya idadi ya majimbo makuu ya Kikatoliki nchini Kenya kufikia tano, yakijumuisha yale ya Nairobi, Mombasa, Kisumu na Nyeri.
Kenya yapata Askofu Mkuu mpya huku Papa akipandisha hadhi Jimbo Kuu la Eldoret
Baada ya kutreuliwa Kasisi Mkatoliki mwaka wa 1996, Obanyi aliteuliwa kuwa Askofu wa Kakamega na Papa Francis mnamo Desemba 2014. / Others

Papa mtakatifu wa kanisa Katoliki Leo XIV amemteua Mhashamu Joseph Obanyi Sagwe kuwa Askofu Mkuu wa kwanza wa Jimbo Kuu la Eldoret, lililoanzishwa hivi karibuni magharibi mwa Kenya.

Uteuzi huo, uliotangazwa na Vatikan Jumamosi, Novemba 14, unafuatia uamuzi wa Papa wa kupandisha hadhi Jimbo la Eldoret na kulifanya kuwa Jimbo Kuu, hatua inayounda jimbo kuu jipya la kanisa hilo nchini Kenya.

Jimbo Kuu jipya la Eldoret litajumuisha majimbo manne tanzu – Lodwar, Kitale, Kericho na Kapsabet – ambayo hapo awali yalikuwa chini ya mamlaka ya majimbo makuu ya Kisumu na Nairobi.

Hatua hii inafanya idadi ya majimbo makuu ya Kikatoliki nchini Kenya kufikia matano, yakijumuisha yale ya Nairobi, Mombasa, Kisumu na Nyeri.

Askofu Mkuu mteule Obanyi, mwenye umri wa miaka 59, hapo awali alihudumu kama Askofu wa Kakamega na aliteuliwa kuwa Msimamizi wa Kitume wa Eldoret kufuatia kuteuliwa kwa Askofu Mkuu Dominic Kimengich kuwa Askofu Mkuu Mwandamizi (Coadjutor Archbishop) wa Mombasa.

Obanyi, ambaye alipewa daraja la upadri mwaka 1996, aliteuliwa kuwa Askofu wa Kakamega na Papa Francis mnamo Desemba 2014. Pia ana sifa za kitaaluma za ngazi ya juu katika Sheria za Kanisa (Canon Law) kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Lateran kilichopo Rome.

Tangazo hilo livutia ujumbe wa pongezi kutoka kwa viongozi wa Kenya na waumini wa Kanisa Katoliki.

Rais William Ruto alikaribisha uteuzi huo, akiuelezea kama fursa ya kuimarisha mchango wa Kanisa katika ustawi wa Wakristo na jamii nje ya eneo la Eldoret.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Kipchumba Murkomen, pia alimpongeza Askofu Mkuu mteule, akisema anatarajia kushirikiana na Kanisa katika kukuza amani, mshikamano wa kijamii, na kuishi pamoja kwa amani katika eneo hilo.

Waumini wa Kanisa Katoliki nao wamepokea hatua hiyo kwa furaha, wakielezea kuwa ni tukio la kihistoria kwa Kanisa na wakati muhimu kwa jumuiya ya Wakatoliki katika eneo hilo.

Kupandishwa huko kwa hadhi kunaashiria mabadiliko makubwa katika muundo wa uongozi wa Kanisa Katoliki magharibi na kaskazini-magharibi mwa Kenya, kwa kuweka majimbo kadhaa ya kikanisa chini ya makao makuu mapya ya jimbo kuu (metropolitan centre) mjini Eldoret.

CHANZO:TRT Afrika and agencies