Wizara ya Elimu ya Uturuki imezitaka shule zote nchini humo kuondoa picha na video za wanafunzi zinazochapishwa hadharani isipokuwa zile zilizoruhusiwa na wazazi, kama sehemu ya utekelezaji wa kanuni mpya yenye lengo la kuimarisha ulinzi wa taarifa binafsi.
Agizo hilo linataka shule kupitia upya mitandao yao na mitandao ya kijamii na kuondoa maudhui iliyochapishwa awali yenye picha za watoto au taarifa binafsi.
Wizara imesema hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaokiuka kanuni hizo.
Wafanyakazi wa shule pia wametakiwa kukamilisha mafunzo ya lazima kuhusu ulinzi wa taarifa binafsi.
Maelekezo haya yanakuja wakati ambapo, baadhi ya walimu nchini Uturuki wamekuwa na idadi kubwa ya wafuasi mitandaoni ikiwemo Instagram, TikTok na YouTube kwa kuweka maudhui ya wanafunzi wakiwa madarasani hivyo kuvutia idadi kubwa wa watu.
Hatua hiyo, imeibua mjadala mpana mitandaoni kwamba inakiuka faragha ya wanafunzi.
Wasiwasi kama huo pia umeibuka kwengine. Nchini Hispania, walimu na wataalamu wa sheria wamekosoa ongezeko la wanaojiita “TeachTokers” kwa kutumia picha za wanafunzi wakiwa madarasani kwa kujinufaisha.
Agizo la Wizara ya Elimu ya Uturuki pia linakuja huku makampuni ya teknolojia yakiangaliwa kwa karibu kuhusu faragha ya mitandaoni.
Wiki iliyopita, Meta iliondoa kipengele kipya cha Instagram kinachotumia Akili Mnemba ambacho kinaruhusu watumiaji kupata picha kutoka kwenye akaunti za watu baada ya kukosolewa kwamba inaibua maswali ya faragha.
Kabla ya kuondolewa, watumiaji wa akaunti za wazi waliingizwa moja kwa moja, ikiwa na maana wengine wangetumia picha zilizopo na kuzibadilisha kwa kutumia Akili Mnemba bila taarifa ya ruhusu wa wamiliki.
Meta baadae ilikiri "kukosea" na kipengele hicho "hakipatikani tena."

















