Waasi wa M23 watishia kulipiza kisasi dhidi ya majeshi ya serikali
Machi 19, 2025, waasi hao walidhibiti mji wa Walikale ulio kaskazini mwa jimbo la Kivu, lakini wakajiondoa ili kutii agizo la kusitisha mapigano lililotolewa Februari 22.
Kikundi cha waasi cha AFC/M23 kimetishia kulipiza kisasi iwapo majeshi ya serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) yataendelea kushambulia raia katika eneo la Walikale.
Kupitia chapisho lake kwenye ukurasa wa X aliloliweka Aprili 3, 2025, msemaji wa kikundi hicho Lawrence Kanyuka, alisema kuwa wapo tayari kujibu mashambulizi iwapo majeshi ya serikali yataendelea kushambulia raia.
“Ikiwa majeshi ya Kinshasa yataendelea na uchokozi wao dhidi ya raia, nasi tuko tayari kukabiliana na vitisho hivyo,” alisema Kanyuka.
Machi 19, 2025, waasi hao walidhibiti mji wa Walikale ulio kaskazini mwa jimbo la Kivu, lakini wakajiondoa ili kutii agizo la kusitisha mapigano lililotolewa Februari 22.
Uamuzi wa kuweka silaha chini, kulingana na waasi hao, ulilenga kuunga mkono jitihada za amani, katika eneo la mashariki mwa DRC.
Katika taarifa yake ya Machi 24, Kanyuka alisisitiza kuwa uwepo wa majeshi ya DRC, yanatatiza jitihada za kumaliza mapigano katika eneo hilo.
Siku ya Alhamisi, gavana wa zamani wa jimbo la Sankuru, Joseph Stephane Mukumadi alijiunga na waasi hao, huku akitoa rai kwa Wakongomani kuungana na kuundoa utawala wa kidikteta nchini humo.
Mukumadi alijiunga na waasi hao siku tano tu baada ya mgombea wa zamani wa urais wa nchi hiyo Rex Kazadi naye kufanya hivyo.