Jeshi la Polisi la Afrika Kusini (SAPS) limesema limeanzisha uchunguzi kufuatia matukio matatu tofauti ya ufyatuaji risasi yaliyotokea jijini Cape Town, Afrika Kusini na kusababisha vifo cya watu wasiopungua 11.
Kwa mujibu wa Polisi matukio hayo yameyotokea katika vitongoji vya Khayelitsha, Langa na Gugulethu Agosti 9, 2026.
Polisi wamesema wanaume watatu wenye umri wa miaka 25, 31 na 35 wamepigwa risasi na kuuawa katika shambulio lililotokea eneo la Lingelethu West, Khayelitsha.
Katika tukio la pili, lililotokea katika Barabara ya Winnie Mandela, eneo la KwaLanga, Langa, wanaume wanne na mwanamke mmoja wameuawa.
Shambulio la tatu lilitokea katika makazi yasiyo rasmi ya Barcelona, Gugulethu, ambapo wanaume wawili na mwanamke mmoja wameuawa, huku watu wengine wawili wakijeruhiwa, kwa mujibu wa polisi.
SAPS imesema vikosi vya ziada vya polisi vimetumwa katika maeneo ambako matukio hayo yalitokea, pamoja na maeneo mengine yanayoonekana kuwa hatarishi.
Kamishna wa Polisi wa Mkoa wa Western Cape, Luteni Jenerali Sizakhele Dyantyi, amesema hadi sasa sababu za mashambulizi hayo hazijabainika. Aliwataka watu wenye taarifa zinazoweza kusaidia uchunguzi kujitokeza na kuwasiliana na polisi.
Dyantyi ametangaza zawadi ya Rand 100,000 za Afrika Kusini sawa na Dola 6,185 za Marekani kwa atakayetoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwa wahusika wa mashambulizi hayo.
Amesema vurugu zinazohusisha magenge na matumizi ya silaha za moto kinyume cha sheria bado ni miongoni mwa changamoto kubwa za kiusalama katika mkoa huo.
















