Raia wa Marekani wamewekwa karantini katika kituo chenye utata cha Ebola nchini Kenya, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Ijumaa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani. Hata hivyo, Waziri wa Afya wa Kenya, Aden Duale amesema hakuwa na taarifa kuhusu hatua hiyo.
Wakenya watatu wamefariki dunia katika maandamano yaliyogeuka kuwa ya vurugu kupinga kuanzishwa kwa kituo hicho cha karantini katika Kambi ya Anga ya Laikipia, iliyoko takriban kilomita 200 kutoka mji mkuu wa Nairobi.
Kenya haijawahi kuripoti maambukizi yoyote ya Ebola, na wananchi wengi wanapinga kuingizwa nchini kwa watu wanaoweza kuwa wameambukizwa ugonjwa huo unaoenea kwa kasi.
Mahakama ya Kenya iliamuru kusitishwa kwa mradi huo na pia imesema Waziri wa Afya, Aden Duale, kuwa amedharau mahakama kwa kutotekeleza mara moja amri ya kuusimamisha.
Hata hivyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilisema katika taarifa kwamba raia kadhaa wa Marekani waliokuwa wakifanya kazi na shirika la Samaritan's Purse katika maeneo yaliyoathiriwa na Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo walihamishiwa katika kituo hicho.
"Hawajapatikana na maambukizi ya Ebola"
"Wahudumu hawa wote wa misaada kutoka Marekani kwa sasa hawaonyeshi dalili zozote za Ebola, na hadi sasa hawajapatikana na virusi vya Ebola baada ya kufanyiwa vipimo," wizara hiyo ilisema.
Iliongeza kuwa walihamishwa kwenda Kenya "kwa tahadhari kubwa tu" na kwamba mamlaka za Kenya ziliruhusu kupelekwa kwao katika kituo hicho.
Hata hivyo, alipoombwa na shirika la habari la AFP kutoa maoni, Waziri wa Afya wa Kenya, Aden Duale alijibu kwa kifupi: "Sina taarifa."
Duale aliiambia mahakama mnamo Juni 23 kwamba alikuwa ameagiza "kusimamishwa mara moja kwa ujenzi wowote uliokuwa umepangwa" wa kituo hicho.
Ukubwa wa maandamano hayo ulisemekana kuwashtua serikali za Kenya na Marekani.
Marekani imeahidi kutoa Dola milioni 13.5 kusaidia juhudi za Kenya za kujiandaa kukabiliana na Ebola. Hata hivyo, wakosoaji pia wanapinga mpango huo wakidai unaashiria mwendelezo wa mtazamo wa kikoloni katika ushirikiano huo.
Rais William Ruto awali alisema ingekuwa "bahati mbaya" kuikataa ombi la kuanzishwa kwa kituo hicho cha karantini, akitaja miongo kadhaa ya msaada wa afya ambao Marekani imekuwa ikiipatia Kenya.
Kwa sasa, Kenya na Marekani zinaendelea kukamilisha makubaliano yenye utata katika sekta ya afya, ambapo Kenya inatarajiwa kutoa kiasi kikubwa cha taarifa za afya, huku Kenya ikipokea msaada wa mabilioni ya dola.














