| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Misri yaishutumu Ethiopia kwa 'kuingiza isiasa' katika uendeshaji wa Bwawa la Mto Nile
Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Badr Abdelatty, amesema usalama wa maji ni suala la "uhai wa taifa," akihimza makubaliano ya kisheria, huku akidai kuwa uendeshaji wa upande mmoja wa bwawa hilo unaathiri upatikanaji wa maji nchini Misri na Sudan.
Misri yaishutumu Ethiopia kwa 'kuingiza isiasa' katika uendeshaji wa Bwawa la Mto Nile
Ethiopia yazindua mradi wa umeme wa maji wa bwaba GERD katika eneo la Guba. / / Reuters

Misri imeishutumu Ethiopia kwa “kuingiza siasa” katika uendeshaji wa Bwawa la Ethiopia (GERD) la Mto Nile kupitia hatua za upande mmoja ambazo zimeathiri Misri na Sudan.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Badr Abdelatty, alitoa kauli hiyo wakati wa mkutano wa pamoja na waandishi wa habari mjini Cairo siku ya Jumatatu akiwa pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Msumbiji, Manuela Lucas.

Abdelatty alisema usalama wa maji ni suala la “uhai wa taifa” na ni kipaumbele cha kitaifa kwa Misri, akisisitiza kwamba “haliwezi kuwekwa rehani wala kuachiwa.”

Alisema Misri imekuwa ikionya mara kwa mara kwamba Ethiopia imeendeleza mradi wa bwawa hilo kupitia hatua za upande mmoja zinazopuuzia sheria za kimataifa na kanuni ya mashauriano ya awali, akiongeza kuwa, “Ethiopia, ikiwa nchi iliyoko sehemu ya juu ya mto, haiwezi kuchukua hatua kwa upande mmoja.”

Pia aliishutumu Ethiopia kwa kuendesha bwawa hilo kwa njia “iliyogeuzwa kuwa ya kisiasa” bila uratibu wa awali na Misri na Sudan, akionya kuwa hatua hizo zimekuwa na “madhara makubwa sana.”

Kupungua kwa kiwango cha maji

Kwa mujibu wa Abdelatty, hatua ya hivi karibuni ya Ethiopia ya kuhifadhi maji bila uratibu wa awali imesababisha kiwango cha maji nchini Sudan kupungua katika siku za hivi karibuni, jambo lililoathiri upatikanaji wa maji kwa jamii za Sudan.

Alisisitiza kuwa Misri “haipingi haki ya Ethiopia ya maendeleo, mradi tu maendeleo hayo yasisababishe madhara kwa Sudan au Misri,” akiongeza: “Wao wana haki ya maendeleo, na sisi tuna haki ya kuishi.”

Misri na Sudan zimekuwa na mvutano wa muda mrefu na Ethiopia kuhusu ujazaji na uendeshaji wa Bwawa la GERD, ambalo Ethiopia ilianza kulijenga mwaka 2011 na kulizindua rasmi mwezi Septemba 2025.

Misri na Sudan zimekuwa zikitaka kuwepo kwa makubaliano ya kisheria yanayowafunga pande zote tatu kuhusu namna ya kujaza na kuendesha bwawa hilo kabla ya mchakato huo kukamilika.

Hata hivyo, Ethiopia inasisitiza kuwa mradi huo hauhitaji makubaliano ya lazima ya kisheria na kwamba haina nia ya kudhuru maslahi ya nchi nyingine yoyote.

Mzozo huo ulisababisha mazungumzo kusimamishwa kwa miaka mitatu kabla ya kuanza tena mwaka 2023, lakini yakakwama tena mwaka 2024.

CHANZO:Anadolu Agency