| Swahili
ULIMWENGU
3 dk kusoma
Trump amsifu Erdogan wa Uturuki kama ‘rafiki mzuri, na kiongozi mahiri’
Trump amemsifu Erdogan kuwa ni “mtu mwenye nguvu sana”, akiongeza kuwa ana urafiki mzuri naye na kwamba viongozi hao wawili wanaheshimiana.
Trump amsifu Erdogan wa Uturuki kama ‘rafiki mzuri, na kiongozi mahiri’
Trump anaangazia uhusiano wake na Rais Recep Tayyip Erdogan. / Picha: Reuters / Reuters

Rais wa Marekani, Donald Trump, ameangazia uhusiano wake na Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, akisema hatarajii kuwepo kwa mvutano kati ya Uturuki na Israel, huku akisisitiza kile alichokitaja kuwa na maelewano ya karibu na kiongozi huyo wa Uturuki.

“Yeye ni rafiki yangu mzuri sana, na tumefanya kazi pamoja kwa mafanikio makubwa. Ninampenda. Ni kiongozi mahiri na mtu mwenye nguvu sana,” Trump aliwaambia waandishi wa habari Jumatano alipoulizwa kuhusu Erdogan wakati wa hafla katika Ofisi ya Oval baada ya kusaini hatua zinazohusiana na usalama wa ndani.

Akijibu swali kutoka kwa mwandishi wa habari wa Israel kuhusu iwapo kunaweza kutokea mzozo kati ya Israel na Uturuki, Trump alipuuza uwezekano huo na kusema angeingilia kati ikiwa itahitajika.

“Sijasikia jambo kama hilo. Kama ningelisikia, ningempigia simu na kuhakikisha kila kitu kiko sawa. Sidhani kama jambo kama hilo litatokea na Uturuki,” alisema.

“Ananiheshimu, nami namheshimu. Zaidi ya hayo, tuna urafiki mzuri.”

Iran

Akizungumzia Iran, Trump alisema Marekani itaendelea na mashambulizi baada ya kile alichokieleza kuwa ni shambulio dhidi ya helikopta ya Apache ya Marekani, ambayo alisema Iran ilikubali kuwa iliidungua.

Alipoulizwa kama Marekani itaendelea na hatua za kijeshi dhidi ya Iran, Trump alijibu bila kusita: “Tutaishambulia, na kwa nguvu kubwa sana,” alisema.

“Ukiangalia shambulio la helikopta, nadhani tuna haki ya kufanya hivyo. Jana tuliipiga pigo kubwa sana, na leo tutatoa pigo lingine kubwa sana.”

“Tutaona kitakachotokea kuhusu makubaliano. Tulikuwa karibu sana kufikia makubaliano, lakini wanaendelea kutuchelewesha; wanaendelea kutufanya wajinga,” alisema.

Trump pia alidai kuwa Marekani imekuwa “ikichukua mamilioni ya mapipa ya mafuta” kupitia operesheni za siri wakati wa vita, akidokeza kuwa lengo kuu lilikuwa kuimarisha bei za soko la dunia.

“Hakuna anayejua hilo. Unajua ni nani hajui kuhusu hilo? Iran, hadi sasa hivi. Usiku mmoja tuliondoa meli 22 usiku wa manane bila taa, kwa sababu hawana rada, kwa kuwa tuliiharibu kabisa mifumo yao,” alisema.

“Hiyo ndiyo sababu mafuta yanauzwa kwa dola 85 kwa pipa.”

Mkataba wa Marekani, Mexico na Canada

Trump alisema hana mpango wa kurdisha Mkataba wa Marekani-Mexico-Canada (USMCA), mkataba wa biashara aliotia saini wakati wa muhula wake wa kwanza.

 “Sina mpango wa kuurudisha,” Trump aliwaambia waandishi wa habari alipoulizwa kuhusu mkataba huo wa biashara wa Amerika Kaskazini.

Alisema kuwa kipengele cha kumalizika kwa mkataba huo kilikuwa mojawapo ya sababu kuu zilizomfanya kuunga mkono kubadilishwa kwa NAFTA na USMCA katika muhula wake wa kwanza.

Trump aliielezea NAFTA kama “mkataba mbaya zaidi wa biashara” ambao Marekani imewahi kusaini, na akasema USMCA ni “mkataba bora zaidi”, hasa kwa sababu unaipa Marekani haki ya kutathmini upya baada ya miaka sita.

“Baada ya miaka sita, unafikia wakati wa kuanzishwa tena. Sijui kama nitauanzisha,” alisema.

Trump alisema Marekani “inafanya vizuri zaidi” bila kutegemea bidhaa kutoka Canada na Mexico, akidai kuwa nchi hizo mbili zinahitaji zaidi soko la Marekani kuliko Marekani inavyohitaji bidhaa zao za kuuza nje.

“Hatujahitaji magari yao; hatuhitaji mbao zao; hatuhitaji nishati yao,” alisema, akiongeza kuwa Marekani inapaswa kuwa na ziada ya biashara na nchi hizo mbili badala ya kuwa na nakisi ya biashara.

 

 

CHANZO:AA