SADC yakosoa mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa Tanzania

Katika taarifa yake ya Jumatatu Novemba 3, ujumbe wa SADC umeainisha baadhi ya changamoto walizokutana nazo wakati wa mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, nchini Tanzania.

Taarifa hiyo ilitolewa mkuu wa ujumbe wa waangalizi wa uchaguzi kutoka SADC, Richard Msowoya./Picha:Wengine / Others

Ujumbe wa Waangalizi wa Uchaguzi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), umesema kuwa Uchaguzi Mkuu wa Tanzania uliofanyika Oktoba 29, 2025, haukuzingatia baadhi ya misingi na kanuni muhimu za uendeshaji uchaguzi ndani ya jumuiya ya SADC.

Ujumbe huo pia ulikosoa namna ulivyapata changamoto ya kukusanya maoni kutoka kwa wadau muhimu wa mchakato huo, wakiwemo kutoka Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), kwa madai kuwa hawakuwa na barua za utambulisho.

Kulingana na SADC, baadhi wa wajumbe walihojiwa na vyombo vya ulinzi na usalama huku, baadhi ya nyaraka zao muhimu kama vile kupokonywa kwa hati zao za kusafiria.

“Walirudishiwa tu baada ya kulazimishwa kufuta baadhi ya picha za mchakato wa uchaguzi kwenye simu zao na vifaa vingine vya kazi,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, baadhi ya wadau walikuwa wanasita kushiriki kutoa taarifa muhimu kwa ujumbe wa SADC, wakiwataka wajumbe hao kufuata maelekezo kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Ujumbe huo, ulidai kuwa kulikuwa na udhibiti mkubwa wa vyombo vya habari siku ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, tofauti na hali ilivyokuwa wakati wa chaguzi zilizopita.

“Baadhi ya wadau walianisha kuwa baadhi ya vyombo vilijidhibiti vyenyewe kwa hofu ya kupoteza leseni iwapo kama namna yao ya kuripoti ingeenda tofauti na matakwa ya serikali,” iliongeza taarifa hiyo.

SOURCE: TRT Afrika Swahili