Trump ameipongeza Congo na Rwanda kwa kusaini mkataba wa amani unaosimamiwa na Marekani
Rais Donald Trump aliwapongeza viongozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Rwanda kwa ujasiri wao walipotia saini makubaliano siku ya Alhamisi yenye lengo la kumaliza mzozo wa mashariki mwa Congo na kutoa fursa ya uchimbaji madini kwa Marekani.
"Ni siku nzuri kwa Afrika, siku kuu kwa ulimwengu," Trump alisema muda mfupi kabla ya viongozi hao kutia saini mkataba huo. Aliongeza, "Leo, tunafaulu ambapo wengine wengi wameshindwa."
Mkataba huo kati ya Rais wa DRC, Felix Tshisekedi na Rais wa Rwanda Paul Kagame unaosifiwa na Ikulu ya White House kama mkataba wa "kihistoria" ulioratibiwa na Trump, unafuatia juhudi za miezi kadhaa za amani za Marekani na washirika wake, ikiwa ni pamoja na Umoja wa Afrika na Qatar, na kukamilisha makubaliano ya awali yaliyotiwa saini mwezi Juni.
Taifa hilo la Congo lililoko Afrika ya Kati limekuwa likikabiliwa na mapigano ya miongo kadhaa na zaidi ya makundi 100 yenye silaha, yenye nguvu zaidi ya waasi wa M23 wanaodaiwa na DRC kuungwa mkono na Rwanda.
Mgogoro huo uliongezeka mwaka huu, huku M23 wakiteka miji mikuu ya eneo hilo ya Goma na Bukavu kwa mwendo ambao haujawahi kushuhudiwa, na hivyo kuzidisha mzozo wa kibinadamu ambao tayari ulikuwa ni mkubwa zaidi duniani, huku mamilioni ya watu wakikimbia makazi yao.
Matumaini ya kudumu kwa amani
Kagame na Tshisekedi walitoa sauti ya matumaini wakati wakitia saini makubaliano hayo.
"Hakuna mtu aliyekuwa akimwomba Rais Trump kuchukua jukumu hili. Kanda yetu iko mbali na vichwa vya habari," Kagame alisema. "Lakini rais alipoona fursa ya kuchangia amani, aliichukua mara moja."
"Ninaamini siku hii ni mwanzo wa njia mpya, njia inayohitaji nguvu nyingi, ndiyo. Hakika, ni ngumu sana," Tshisekedi alisema. "Lakini hii ni njia ambayo amani haitakuwa tu matarajio, bali hatua ya mabadiliko."
Naye Trump alitabiri kwa kutia saini nchi hizo zitaacha nyuma "miongo kadhaa ya vurugu na umwagaji damu" na "kuanza mwaka mpya wa maelewano na ushirikiano."
"Walitumia muda mwingi kuuana," Trump alisema. "Na sasa watatumia muda mwingi kukumbatiana, kushikana mikono na kuchukua fursa ya Marekani ya kiuchumi kama kila nchi nyingine."