Rais William Ruto wa Kenya ameuomba Umoja wa Ulaya (EU) na mamlaka za kimataifa kusaidia kuiondoa Kenya kwenye orodha ya nchi zenye hatari kubwa ya utakatishaji fedha na ufadhili wa kigaidi.
Kiongozi huyo, ametoa ombi hilo Novemba 12, 2026, wakati alipokutana na wakuu wa ujumbe wa EU kutoka nchi mbalimbali za Afrika, jijini Nairobi.
Kulingana na Rais Ruto, Kenya imefanikiwa kutekeleza na kumaliza mapungufu 13 kati ya 21 yaliyotambuliwa na FATF katika mifumo yake ya kifedha.
Aliongeza kuwa, uamuzi wa kuiondoa Kenya katika orodha hiyo, utapunguza vikwazo na ukaguzi wa ziada, unaowakabili wafanyabiashara wa Kenya, miamala ya benki, na upitishaji wa fedha za wakenya walioko nje ya nchi hiyo.
Kenya iliwekwa kwenye orodha ya nchi zenye hatari kubwa za utakatishaji fedha ya Umoja wa Ulaya kuanzia Agosti 5, 2025.




















