Mikakati hiyo ilihusisha mageuzi ya kina katika sekta ya afya, ikiwa ni pamoja na miundombinu, teknolojia, elimu ya tiba, ubora wa huduma, bima ya afya kwa wote pamoja na ushiriki wa wananchi katika kujikinga dhidi ya magonjwa.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano la kitaifa la madaktari jijini Dar es Salaam,Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dkt. Mugisha Nkoronko alisema kongamano hilo la kila mwaka limekuja katika kipindi muhimu ambapo Tanzania imekamilisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na sasa inaanza safari ya utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050.
Alisema kaulimbiu ya kongamano hilo "Huduma za Afya Tunazozitaka Mwaka 2050," inalenga kutoa mchango wa kitaalamu kuhusu namna sekta ya afya itakavyoweza kusaidia taifa kufikia malengo ya maendeleo yaliyowekwa katika dira mpya.
Dkt. Nkoronko alisema katika kipindi cha miaka 25 iliyopita Tanzania imepiga hatua kubwa katika sekta ya afya kutokana na uwekezaji uliofanywa na Serikali pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo.
“Mafanikio hayo yameonekana katika kupungua kwa vifo vya akina mama wajawazito na watoto, kupungua kwa vifo vinavyotokea kabla ya umri wa kuishi, pamoja na kuongezeka kwa wastani wa umri wa kuishi wa Mtanzania kutoka takribani miaka 50 mwaka 2000 hadi kufikia wastani wa miaka 60 kwa sasa.
Alifafanua kuwa kwa sasa wanawake nchini wana wastani wa kuishi hadi miaka 66 huku wanaume wakifikia wastani wa miaka 64, jambo linaloonesha mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha robo karne iliyopita.Hata hivyo amesema matarajio ya Dira ya Taifa 2050 ni kuona Watanzania wanaishi wastani wa miaka 75, lengo ambalo haliwezi kufikiwa bila kuimarisha zaidi mfumo wa afya nchini.
Aidha alisema dira hiyo inalenga pia kujenga uchumi wa dola trilioni moja za Marekani huku kila Mtanzania akitarajiwa kuwa na kipato cha wastani cha dola za Marekani 7,000 kwa mwaka ifikapo mwaka 2050. Kwa mujibu wake, malengo hayo hayawezi kufikiwa kama taifa halitakuwa na wananchi wenye afya njema na mfumo imara wa utoaji wa huduma za afya.
Alisema madaktari na wataalamu wa afya wamekubaliana kuwa jambo la kwanza linalopaswa kupewa kipaumbele ni kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya kutolea huduma za afya pamoja na vifaa vya kisasa vya uchunguzi na tiba.
Alisema ifikapo mwaka 2050 kila hospitali ya wilaya inapaswa kuwa na vifaa vya kisasa vinavyopatikana katika hospitali kubwa ili wananchi wasilazimike kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za kibingwa.
Alisisitiza kuwa daktari anapomwona mgonjwa anapaswa kuwa na uwezo wa kufanya uchunguzi sahihi kwa kutumia vifaa vya kisasa vinavyoendana na maendeleo ya teknolojia duniani.
"Nia yetu ni kuhakikisha mwaka 2050 daktari anapomwona mgonjwa awe na uhakika wa kile anachokitibu kwa sababu vifaa vya uchunguzi vitakuwa vya kisasa, sahihi na vinavyokidhi mahitaji ya wakati," alisema.
Mgeni Rasmi katika Kongamano hili Katibu Mkuu wa Wizara ya afya akimwakilisha waziri wa Afya,Mohammed Mchengerwa amesema serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika miundombinu watu wengi wanapata huduma za afya maeneno mbalimbali kwa kuendelea kuwekeza vifaa tiba,miundombinu na vifaa vya kiafya ambapo asilimia 90 ya hospitali nchini zina digital X-Ray na Ultrasound.
“Na pia serikali inawekeza katika huduma za kibingwa na ndio maana Rais ametoa fellowship (Samia Scholarship) kuhakikisha watanzania ifikapo 2050 hawatasafirishwa nchi za nje kupata huduma kwa uwekezaji mkubwa hii inawezakana kupunguza vifo vya uzazi.








