Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, amezungumza kuhusu masuala ya kikanda na marais wa Rwanda, Paul Kagame, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Félix Tshisekedi, kupitia mazungumzo ya njia ya simu, kwa mujibu wa Kurugenzi ya Mawasiliano ya Uturuki.
Katika mazungumzo yake na Tshisekedi siku ya Alhamisi, viongozi hao walijadili uhusiano wa mataifa mawili na njia za kuimarisha ushirikiano kati ya Uturuki na DRC.
Erdogan amesema Uturuki itaendelea kuchukua hatua za kuimarisha ushirikiano na DRC katika maeneo mbalimbali, hususan uwekezaji, biashara, sekta ya ulinzi na usalama.
Pia alieleza kuunga mkono michakato iliyoanzishwa kwa lengo la kufikia suluhisho la kudumu na la amani kuhusu hali ya usalama katika mashariki mwa DRC.
Rais Erdogan amesema Uturuki iko tayari kutoa “mchango unaohitajika katika kuunda mazingira yenye kujenga kwa ajili ya utekelezaji wa makubaliano yaliyopo.”
Katika mazungumzo yake tofauti na Rais Kagame, Erdogan alibainisha kuwa kumekuwa na maendeleo chanya katika biashara na uwekezaji kati ya Uturuki na Rwanda.
Amesema Uturuki itaendelea kushirikiana na Rwanda katika maeneo mbalimbali, hususan sekta ya ulinzi.
Erdogan pia amepongeza juhudi za kupunguza mvutano kati ya Rwanda na DRC, pamoja na kuendelea kwa mtazamo wa kujenga kati ya nchi hizo mbili.
Aidha, amesisitiza tena kwamba Uturuki inaunga mkono mchakato unaolenga kupunguza mvutano na kufanikisha amani ya kudumu katika eneo hilo.























