Vikosi vya Iran (IRGC) vimesema kuwa vimeshambulia kambi ya jeshi la Marekani nchini Kuwait kujibu shambulio la anga la Marekani lililofanyika karibu na Uwanja wa Ndege wa Bandar Abbas kusini mwa Iran.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Tasnim la Iran, IRGC imesema shambulio hilo la kulipiza kisasi lilifanyika saa 10:50 alfajiri ya Alhamisi, saa chache baada ya kile ilichokiita mashambulizi ya Marekani kwenye eneo la karibu na uwanja wa ndege wa mji huo wa bandari kwa kutumia makombora ya anga.
“Hili ni onyo kali ili adui ajue kuwa uchokozi hautaachwa bila kujibiwa, na ukirudiwa, jibu letu litakuwa kali zaidi,” ilisema.
Hadi sasa hakuna ufafanuzi kutoka kwa jeshi la Marekani kuhusu shambulio hilo.
Mapema siku hiyo, afisa mmoja wa Marekani alisema kuwa vikosi vya Marekani vilidungua ndege nne zisizo na rubani za Iran ambazo zilikuwa tishio karibu na Mlango-Bahari wa Hormuz, na pia vilishambulia kituo cha udhibiti wa ardhini huko Bandar Abbas ambacho kilikuwa kikijiandaa kurusha ndege ya tano isiyo na rubani.
“Hatua hizi zilikuwa za kiwango kiasi, za kujilinda pekee, na zililenga kudumisha usitishaji wa mapigano,” alisema afisa huyo ambaye alizungumza kwa sharti la kutotajwa jina.
‘Uvunjaji mkubwa wa usitishaji wa mapigano’
Mashambulizi hayo ya karibuni yalikuja baada ya Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM) kuthibitisha mapema wiki hii duru nyingine ya mashambulizi kusini mwa Iran yaliyolenga maeneo ya kurushia makombora na boti za Iran zilizodaiwa kuwa zilikuwa zikijaribu kuweka mabomu ya majini. Iran ililaani mashambulizi hayo kama “uvunjaji mkubwa wa usitishaji wa mapigano.”
Awali, akizungumzia hali ya mazungumzo ya kumaliza vita dhidi ya Iran, Rais wa Marekani Donald Trump alisema kuwa “haridhishwi nayo, lakini tutaridhika. La sivyo, tutalazimika kumaliza kazi hiyo.”
Mvutano wa kikanda uliongezeka mnamo Februari 28 wakati Marekani na Israel zilipoanzisha mashambulizi ya kushtukiza dhidi ya Iran, na kuifanya Iran kujibu kwa mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na makombora yaliyolenga maeneo mbalimbali katika ukanda huo pamoja na kufunga Mlango-Bahari wa Hormuz.
Usitishaji wa mapigano ulianza kutekelezwa Aprili 8 kupitia upatanishi wa Pakistan, lakini mazungumzo huko Islamabad hayakufanikiwa kufikia makubaliano ya kudumu.
Baadaye, Trump aliongeza muda wa usitishaji wa mapigano bila kikomo huku akiendelea kuweka vizuizi kwa meli za Iran kwenda au kutoka bandari za Iran kupitia njia hiyo muhimu ya majini, na mara kwa mara kusema kuwa makubaliano ya amani yalikuwa karibu kufikiwa.















