DRC yatangaza kumalizika kwa ugonjwa wa Ebola
Mamlaka ya afya katika Jamhuri ya Kidomokrasia ya Congo siku ya Jumatatu ilitangaza kumalizika kwa mlipuko wa hivi punde wa ugonjwa wa Ebola, ambao umesababisha takriban vifo 34 tangu Agosti.
Virusi hivyo vimesababisha vifo 15,000 barani Afrika katika miaka 50 iliyopita.
Mlipuko mbaya zaidi nchini DR Congo kati ya 2018 na 2020 uliua karibu watu 2,300 kati ya 3,500 walioambukizwa.
Mkuu wa Taasisi ya Kitaifa ya Afya ya Umma (INSP), Dieudonne Mwamba Kazadi, alisema mlipuko huo "umekwisha" mbele ya waliohudhuriaa sherehe rasmi huko Kinshasa.
Kazadi alisema kumekuwa na vifo vya angalau 34 kutoka kwa maambukizi 53 yaliyothibitishwa. Vifo vingine 11 vinaonekana kusababishwa na virusi hivyo, na kuchukua jumla ya vifo kufikia 45, aliongeza.
DR Congo imekuwa na milipuko 16 ya Ebola tangu virusi hivyo vilipotambuliwa kwa mara ya kwanza mwaka 1976, wakati nchi hiyo kubwa ya Afrika ya kati ilipojulikana kama Zaire.
Mlipuko wa mwisho, katika jimbo la kati la Kasai, ulianza Agosti 20, wakati mwanamke mwenye umri wa miaka 34 alilazwa hospitalini.
Mamlaka ya Congo ilitangaza rasmi kuzuka kwa ugonjwa huo mwanzoni mwa Septemba.
Usambazaji wa chanjo
Aidha, mpango wa chanjo ulianza katikati mwa Septemba.
Kundi la Kimataifa la Kuratibu (ICG) kuhusu Utoaji wa Chanjo, ambalo linasimamia hisa za kimataifa, lilituma dozi 45,000 za ziada za dawa za Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Maambukizi ya Ebola kwa binadamu hutokea kupitia majimaji ya mwili. Dalili kuu ni homa, kutapika, kutokwa na damu na kuhara.
Virusi huambukiza tu wakati dalili zinaonekana baada ya muda wa incubation wa siku mbili hadi 21.