Mamlaka za serikali nchini Tanzania, kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama vimefanikiwa kukamata madini ya dhahabu yenye thamani ya Bilioni 1.3 yaliyokuwa yakitoroshwa kwenda nje ya nchi kinyume cha sheria.
Kukamatwa kwa madini hayo kumeripotiwa kufuatia operesheni ya Julai 1, 2026 iliyofanywa na Jeshi la Polisi, Tume ya Madini kwa kushirikiana na vyombo vya Ulinzi na Usalama na Kikosi Kazi cha Kuzuia Utoroshaji wa Madini.
Baada ya utambuzi na uthamanishaji kufanyika ilibainika kuwa idadi ya vipande vya dhahabu vilivyokuwa vikitoroshwa ni 163 vyenye uzito wa gramu 4434.66.
Akizungumza na vyombo vya habari, Naibu Waziri wa Madini wa nchi hiyo, Dkt. Steven Kiruswa, amesema kuwa, serikali ya Tanzania imejipanga vyema kuendelea kusimamia sekta ya madini ili kukabiliana na utoroshaji wa madini unaofanywa na watu ambao sio waaminifu.
Kulingana na waziri huyo, katika kipindi cha mwezi Julai 2025 hadi Machi 2026 , Tanzania imefanikiwa kukamata madini yenye thamani ya Bilioni 3.31 ambayo yalikamatwa katika matukio 55 nchini humo.
Aidha, ametoa wito kwa wachimbaji, wafanyabiashara wa madini, na wananchi kwa ujumla kutumia masoko rasmi zaidi ya 40 ya madini na vituo vya ununuzi vilivyoanzishwa kote nchini ili kufanya biashara zao kwa usalama, uhuru, na kuchangia maendeleo ya taifa.













