| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Kauli ya Makamu wa Rais Tanzania kuhusu Katiba mpya ilivyoibua mjadala
Wadau mbalimbali, ikiwemo wanasiasa kutoka chama tawala CCM na upinzani, pamoja na viongozi wa dini baadhi yao wameibuka na kuikosoa kauli hiyo huku wengine wakiitilia shaka.
Kauli ya Makamu wa Rais Tanzania kuhusu Katiba mpya ilivyoibua mjadala
Baadhi ya wadau wameibuka na kuikosoa kauli hiyo huku wengine wakiitilia mashaka. Picha/Ofisi ya Makamu wa Rais

Siku moja tu baada ya Makamu wa Rais nchini Tanzania Emmanuel Nchimbi kuwataka raia wa nchi hiyo kupigania katiba mpya, na kusema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan yuko tayari mchakato huo kuanza, kauli hiyo inaonekana kuibua mjadala mpana miongoni mwa wananchi.

Wadau mbalimbali, ikiwemo wanasiasa kutoka chama tawala CCM na upinzani, pamoja na viongozi wa dini baadhi yao wameibuka na kuikosoa kauli hiyo huku wengine wakiitilia shaka.

Rajabu Maganya, Mwenyekiti wa Jumuia ya Wazazi ya CCM na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) amehoji iwapo kuna aliyezuia mchakato wa Katiba mpya kwa kuuliza, "Ni nani amesema hakutakuwa na Katiba mpya?" huku akisisitiza kuwa, Serikali ya CCM haijawahi kutangaza kuwa mchakato huo hautafanyika.

Maganya amenukuliwa akitoa kauli hiyo Julai 24, 2026, jijini Dar es Salaam. Kauli yake inakuja muda mfupi tu baada ya kauli ya Makamu wa Rais Emmanuel Nchimbi ya kuwataka Watanzania wakomae katika kudai Katiba mpya, ambayo aliitoa alipokuwa mgeni rasmi katika Mkutano Mkuu wa 15 wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) uliofanyika Julai 24, jijini Dar es Salaam.

Nae Mwenyekiti wa Jumuia ya Vijana wa CCM (UVCCM) Mohamed Kawaida, kupitia ukurasa wake wa kijamii alinukuliwa na vyombo vya habari nchini humo akisema kuwa uimara wa chama hauko katika uwezo wa kiongozi mmoja kujijengea taswira mbele ya umma bali katika uwezo wa taasisi kusimamia nidhamu, kulinda maamuzi yake ya pamoja na kuhakikisha kuwa uongozi unabaki kuwa wa taasisi badala ya kuwa wa mtu mmoja.

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini Tanzania, wameziona kauli hizi kutoka kwa viongozi wa CCM kama kutofurahishwa na kauli iliyotolewa na Makamu wa Rais.

Nae Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, Benson Bagonza, amehoji kauli ya Julai 24, 2026 ya Makamu wa Rais ya kuwataka Watanzania wapambane kupata katiba mpya akisema, "Ikiwa hitaji la katiba mpya ni takwa la Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kama alivyosema Dkt. Nchimbi, kuna haja gani ya wananchi kupambana ili waipate katiba hiyo mpya na ni nani wanapaswa kupambana naye ili waipate."

Katika mahojiano na Saut Digital, Askofu Bagonza amesema, "Kama Rais anaitaka kwa nini tuipambanie. Swali la pili, tunapambana na nani ili kuipata? Swali la tatu, Makamu kusema ni jambo zuri, lakini anaposema Rais anaitaka, kwa nini Rais mwenyewe hasemi moja kwa moja?"