Moto wa nyika, uliokuwa ukitishia maeneo ya makazi katika mji wa Kruja, katikati mwa Albania, ulidhibitiwa baada ya operesheni ya kuzima moto iliyohusisha pia ndege ya Uturuki isiyo na rubani aina ya Bayraktar TB2.
Moto umeibuka katika maeneo mbalimbali nchini Albania katika siku za hivi karibuni, ikiwa ni pamoja na moto mkubwa ulioteketeza maeneo ndani na pembezoni mwa mji wa Kruja, ulio katika eneo la milimani karibu na mji mkuu, Tirana.
Operesheni ya kuzima moto iliendelea usiku kucha mjini Kruja, ikihusisha takribani watu 300 kutoka Jeshi la Wanajeshi, vikosi vya kukabiliana na hali dharura za kiraia pamoja na Idara ya Zimamoto.
Mamlaka zilisema Jumapili kwamba operesheni za kuzima moto kutoka angani pia zilifanyika katika eneo hilo.
Operesheni hiyo ilihusisha magari 21 ya kuzima moto, helikopta tatu, ndege moja isiyo na rubani aina ya Bayraktar TB2 na ndege mbili zisizo na rubani zenye uwezo wa kutumia teknolojia ya picha za joto kubaini maeneo yenye joto kali.
Baadhi ya wakazi walihamishwa kutoka kwenye makazi yaliyoathiriwa na moto huo.
Baada ya moto huo kudhibitiwa, Waziri Mkuu wa Albania, Edi Rama, aliandika katika chapisho kwenye mtandao wa X kwamba ghala moja liliteketea kwa moto, lakini hakuna aliyejeruhiwa.
Rama alisema: “Katika mapambano makali dhidi ya moto katika Mlima Kruja, vifaa vya kuzima moto kutoka angani vilitumika usiku kucha kutokana na upepo. Wazima moto wetu, wanajeshi na vikosi vya polisi walipambana kwa ushujaa na weledi mkubwa, na kuzuia hali hiyo kugeuka kuwa janga, kama ilivyotokea katika nchi nyingine za Ulaya katika kipindi hiki cha kiangazi chenye joto kali.”
Waziri wa Mambo ya Ndani, Besfort Lamallari, amefuatilia operesheni ya kuzima moto akiwa eneo la tukio.
Lamallari aliwaambia waandishi wa habari kwamba moto huo haukusababishwa na sababu za kiasili, bali ulisababishwa na binadamu. Aliongeza kuwa polisi wamemkamata mshukiwa mmoja.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Taasisi ya Sayansi za Jiolojia ya Albania, baadhi ya miji nchini humo bado ilikuwa katika kiwango cha “hatari kubwa” ya kukumbwa na moto wa nyika siku ya Jumapili.
Mwaka 2025, Bayraktar TB2, ndege ya kivita isiyo na rubani (UCAV) iliyotengenezwa nchini Uturuki na kampuni ya Baykar Technologies, iliweka historia katika anga baada ya kuwa ndege ya kwanza isiyo na rubani kufanikiwa kufanya maneva ya kiotomatiki ya kurejesha udhibiti wa ndege kutoka kwenye mzunguko wa kupoteza udhibiti.
Katika jaribio la safari, ndege hiyo iliwekwa kwa makusudi katika hali ya kuzunguka huku ikipoteza udhibiti.
Kwa kutumia mifumo yake ya hali ya juu ya udhibiti, iliweza kujirekebisha yenyewe na kurejea katika safari thabiti na iliyo sawa.
Maneva hiyo ilikuwa haijawahi kufanikiwa kufanywa na ndege nyingine yoyote ya kivita isiyo na rubani (UCAV).






















