Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki ametoa wito wa kufanyika kwa mageuzi makubwa ndani ya Baraza la Usalama wa Mataifa, ikiwemo kuondoa kura ya turufu.
Erdogan amesisitiza kuwa haja ya Baraza hilo kuendana na mfumo wa uanzishwaji wake, baada ya Vita Kuu ya Pili ya dunia.
Erdogan alisisitizia umuhimu wa kuwa na mfumo fanisi wa uwakilishi wakati wa kutoa maamuzi.
Hali kadhalika, alitoa wito wa kufanyika mageuzi makubwa, akitoa kauli mbiu ya ‘Dunia ni zaidi ya mataifa matano’.
Kwa miaka mingi sasa, baraza hilo limekosolewa kwa kuwa na wanachama watano wenye kura ya turufu, ambao ni Marekani, Uingereza, Ufaransa, Urusi na China.
"Ni muhimu kuwa na mageuzi ambayo pia yataondoa utaratibu wa kura ya turufu."
Alibainisha kuwa, uongezaji wa wanachama wapya ndani ya baraza hilo, si suluhu.
‘Nafasi ya kipekee ya baraza hilo'
Rais huyo, pia ametaka kuwepo kwa uwiano mpya kati ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Baraza Kuu.
Ametaka kuongezwa nguvu kwa Baraza Kuu na kuundwa kwa Baraza la Usalama bila uwepo wa wanachama wa kudumu, ambao watachaguliwa na Baraza Kuu.
Kupitia mpangilio huo, Erdogan alisema nchi ambazo zitakuwa zinawania nafasi hizo, zitachaguliwa kwa njia ya kura.
"Ni vyema kuongeza uwakilishi na uwajibikaji wa Baraza la Usalama mbele ya Baraza Kuu,” alishauri.
Kulingana na Erdogan, zimeibuka baadhi ya taasisi mbalimbali zenye nguvu za kiuchumi, kiteknolojia na kidiplomasia, huku taasisi zikishindwa kufikia malengo yao.
Alibainisha kuwa, vita na mabadiliko ya tabia nchi na uhamaji wa watu, umeonesha umuhimu wa taasisi hizi.
Kulingana na Erdogan, bara la Asia linazidi kuelemewa na mzigo, huku nchi Afrika zikitafuta uwakilishi kutokana na fursa zilizopo ndani ya bara hilo.
Wito wa kuwepo na usawa wa kiuchumi ulimwenguni
Erdogan amesema kuwa nchi zinazoendelea zinaendelea kupaza sauti kwa ajili ya vipaumbele vyao, akiongeza kuwa matatizo ya kikanda hayatotatuliwa na watu wa nje.
Amezitaka nchi zenye uwezo wa kidiplomasia na kiuchumi, kuwa mstari wa mbele katika kukuza amani na utulivu.
Ameongeza kuwa, tofauti za kiuchumi, zimeongeza utegemezi wa teknolojia na kiuchumi.
Kiongozi huyo, amebainisha kuwa, Uturuki itaendelea kutumia uzoefu wake kuleta mageuzi katika mifumo ya kimataifa.
Alisema kuwa ushirikiano kati ya nchi kutoka maeneo mbalimbali, ukizingatia kanuni za pamoja, ungeimarisha uhalali na uwezo wa mfumo wa kimataifa wa kuwakilisha wadau.
"Amani ya kudumu katika ulimwengu wa leo haiwezi kupatikana kwa kuongeza idadi ya kambi ambazo hazina uhusiano na hazishirikiani," alisema Erdogan.
"Ili kuwa na ulimwengu wenye haki zaidi, ni lazima tuunganishe uzoefu, uwezo na utashi wa maeneo mbalimbali katika msingi wa pamoja."
Erdogan alisema Uturuki itaendelea kutekeleza wajibu wake katika juhudi za kuufanyia marekebisho mfumo wa kimataifa, akirejelea utamaduni wa kitaifa wa nchi hiyo, uwezo wake wa kidiplomasia na uhusiano wake na maeneo mbalimbali.






















