Waziri Mkuu Tanzania aahidi kuboresha bajeti ya elimu

Amesema Serikali itaendelea kuboresha bajeti ya elimu wakati ikitekeleza mtaala mpya wa elimu ili kuziba mianya ya mahitaji shuleni.

By
Waziri Mkuu wa Tanzania Mwigulu Nchemba. Picha/PMO / TRT Afrika Swahili

Waziri Mkuu Tanzania Mwigulu Nchemba amesema Serikali itaendelea kuboresha bajeti ya elimu wakati ikitekeleza mtaala mpya wa elimu ili kuziba mianya ya mahitaji shuleni.

“Kwa kuwa tunaenda katika mtaala mpya wa elimu, tutaendelea kuboresha bajeti kwa sababu mahitaji yanaongezeka kila wakati katika kumfanya mtoto asome vizuri,” amesema.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo Bungeni jijini Dodoma, Aprili 9, 2026 wakati akijibu swali la Mbunge wa Segerea, Agnesta Lambert Kaiza, kwenye kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu ambaye alitaka kujua kauli ya Serikali juu ya kukomesha michango holela inayotozwa shuleni.

Waziri Mkuu amesema Serikali haina shida na michango ya chakula ambayo imekuwa ikitolewa shuleni lakini akasisitiza kuwa endapo kutatokea michango mingine yoyote, ni lazima ifuate miongozo ya serikali na ipate baraka za Wakuu wa Mikoa husika.