Zimbabwe: Marekebisho ya katiba au kifumba macho?
Mswada wa Marekebisho ya Katiba Na. 3 (2026) unaleta mabadiliko makubwa ikijumuisha mihula iliyorefushwa ya Rais na Wabunge kutoka miaka 5 hadi 7
Emmerson Mnangagwa amekuwa rais wa Zimbabwe katika awamu mbili muhimu - kwanza kupitia kipindi cha mpito wa kisiasa, kisha kupitia uchaguzi.
Novemba 2017, kiongozi wa muda mrefu Robert Mugabe alilazimika kujiuzulu baada ya kuingilia kati kwa msaada wa kijeshi.
Mnangagwa, ambaye alikuwa amefukuzwa kazi kama makamu wa rais, alirejea na kuapishwa kuwa Rais. Huu ulikuwa uhamishaji wa madaraka, sio uchaguzi.
Alipokuwa akifanya kampeni za kuwania urais, ilikuwa kwenye jukwaa la demokrasia, kudumisha katiba na kumaliza muda mrefu wa urais uliokita mizizi.
Uchaguzi kusongeshwa mbele
Kwa hivyo mwaka 2018 alishinda kwa muhula wake wa kwanza na kisha akashinda tena mwaka 2023 kwa muhula wake wa pili na wa mwisho kwa mujibu wa katiba ambao unamalizika 2028.
Lakini sasa, anataka kubadilisha katiba ili kumruhusu kuongeza muda wake wa kukaa madarakani.
Mswada wa Marekebisho ya Katiba Na. 3 (2026) unaleta mabadiliko makubwa ikijumuisha mihula mirefu zaidi, hiyo ni kwa kipindi cha urais: kutoka miaka mitano hadi saba, hii ni kwa wabunge pia, ambapo iwapo pendekezo hilo litapita, basi wataongezewa muda hadi miaka saba kutoka mitano.
Mabadiliko haya vile vile yatasogeza mbele mwaka wa uchaguzi kutoka 2028 hadi 2030 ili kutoa muda wa kutosha wa maandalizi.
Marekebisho yanazunguka sheria
Rais Mnangagwa hivyo atasalia madarakani hadi 2030 kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu.
Sehemu ya mapendekezo ya mabadiliko ni pamoja na kuhama kutoka kwa kura ya moja kwa moja ya umma hadi uchaguzi wa bunge, kutaleta mamlaka zaidi ya utendaji, kuongezeka kwa udhibiti wa taasisi na kupanua mamlaka ya uteuzi.
Lakini katiba ya Zimbabwe inasema, huwezi kubadilisha ukomo wa mihula kwa njia ambayo inamnufaisha rais aliyepo bila kura ya maoni. Wakosoaji wanasema marekebisho haya yanajaribu kuizunguka sheria.
Viongozi wa upinzani na mawakili wa katiba wamekwenda mahakamani kujaribu kuizuia wakisema hatua hiyo ni kujaribu kung'ang'ania madaraka, inadhoofisha demokrasia na kwa kuongeza muda: ‘uchaguzi usipofanyika kwa muda inapunguza uwajibikaji.’
Uamuzi wa mahakama
Hata hivyo, serikali inahoji kuwa kurefusha muhula kunaruhusu upangaji wa uchumi wa muda mrefu na kuiepusha nchi kuingia katika uchaguzi wa mara kwa mara ambao unadaiwa kuvuruga sera.
Kwa upande wake, wafuasi wa Mnangagwa wanasema anahitaji muda zaidi ili kuleta utulivu wa uchumi na kuendeleza miundombinu na mafanikio ya kilimo.
Vuta nikuvute hii inanaendelea huku uamuzi wa mahakama ukusubiriwa, lakini wale wanaofuatilia kutoka ndani na nje ya Zimbabwe wamebaki na swali, Je, hii ni kuhusu utulivu... au kubaki madarakani?