Kila mwaka ulimwengu hushangazwa na uhamaji wa takriban nyumbu mamilioni kutoka Tanzania kwenda Kenya na kurudi, wakivuka mto Mara.
Hata hivyo, unajua jinsi maisha ya wanyama hao yanavyoanza?
Kwa kweli huanza sasa kati ya mwezi wa Februari na Machi huko nchini Tanzania.
Kati ya Januari na Machi mtu anaweza kuona jinsi wanyama hawa wanaavyozaliwa katika sehemu inayojulikana maarufu kama Ndutu, ambayo iko katika eneo la Hifadhi ya Ngorogoro.
Kwa kawaida nyumbu jike ambaye anabeba mimba kwa muda wa miezi 8 hadi 8 na nusu atakuwa anajifungua.
Yeye huzaa akiwa katikati ya kundi ambapo wanyama wengine wote wanashuhudia. Hii inasaidia kutoa ulinzi kwa ndama ambao mara nyingi wanakabiliwa na hatari ya kushambuliwa na wanyama wengine.
Hii ni tofauti na wanyama wengine ambao hujificha wakati wa kuzaa.
Takriban 85% ya ndama huzaliwa katika msimu huu wa mvua ndani ya pengo la wiki 2 hadi 3.
Ndama huwa na uzito wa kati ya kilo 20 hadi 22 wakati wa kuzaliwa na hujifunza kutembea ndani ya dakika chache baada ya kuzaliwa, chini ya wiki moja anakuwa tayari sehemu ya msafara wa nyumbu wengine.
Wanapozaliwa, wanakuwa na rangi ya manjano au kahawia hivi, lakini rangi hubadilika na kuwa ya nyumbu wa kawaida ndani ya miezi miwili.
Ndama huanza kula nyasi kwa siku 10 huku wakiendelea kunyonya hadi miezi 4 hadi 6.
Wanaachishwa kunyonya wakiwa na miezi 6 hadi 9.
Ndani ya miezi 16 ndama wengi wanakuwa tayari wamekuwa kuanza kujamiiana.
Ndama wengi hukaa na mama zao hadi pale ndama mwingine atakapozaliwa.
Majike hukaa kwenye kundi moja na mama huku madume wakiondoka wakiwa miezi 8 kwenda kuungana na kuunda vikundi na wale wa rika lao.
Baada ya Machi msimu wa kuzaa huwa imekwisha na hapa nyumbu sasa wanaanza kuelekea magharibi mwa Seronera na Mto Grumeti katika tambarare ya kaskazini ya Serengeti inayopakana na Maasai Mara ya Kenya wakiwa tayari kuvuka.
Kwa hivyo usisubiri tu wanyama wanapokuwa wamekomaa na kuvuka mto Mara kuingia Kenya katika miezi ya Julai hadi Agosti, unaweza kushuhudia pia mwanzo wa maisha yao wakati huu.















