Hamas yataka Iran kuacha kushambulia nchi jirani
Hamas, ambayo ilipigana na Israel kwa miaka miwili Gaza, pia imetaka jumuia ya kimataifa "kushirikiana kusitisha" mapigano haraka.
Kundi la wapiganaji la Palestina Hamas limeitaka Iran kujizuia kushambulia nchi jirani, huku ikisisitiza haki ya Iran ya kujitetea dhidi ya Israel na Marekani.
Katika wito wa kipekee uliotolewa Jumamosi, Hamas pia imeitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua za kusitisha mapigano yaliyoikumba Mashariki ya Kati tangu Februari 28.
"Tunaposisitiza haki ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kujibu mashambulizi kwa namna yote kwa mujibu wa taratibu na sheria za kimataifa, kundi hilo linawataka ndugu zake wa Iran kuacha kulenga nchi jirani," Hamas imesema katika taarifa yake, wito huo ni wa kwanza kutolewa hadharani kwa Iran.
Hamas, ambayo ilipigana na Israel kwa miaka miwili Gaza, pia imetaka jumuia ya kimataifa "kushirikiana kusitisha" mapigano haraka.
Kundi hilo awali lililaani mauaji ya aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa Iran, Ali Khamenei, yaliyofanyika siku ya kwanza ya mapigano na kuyaita "uhalifu mbaya," ikitambua wazi uugaji mkono wake kwa kundi hilo la Palestina.
"Alitupa msaada wa kisiasa, kidiplomasia na kijeshi, malengo yetu, na ukakamavu wetu," kundi hilo lilisema punde tu baada ya kuuawa kwa Khamenei.
Afisa mmoja wa Hamas ameiambia AFP kwamba wamekuwa katika mawasiliano na maafisa wa Iran kuhusu suala hilo.
"Israeli inataka kupanda mbegu ya chuki kati ya Iran na nchi jirani za Kiislamu," kimesema chanzo hicho, kilichozungumza kwa misingi ya kutotajwa.
Licha ya mashambulizi ya Marekani na Israel, Iran imekuwa ikilipiza kisasi kwa makombora na droni dhidi ya nchi takriban 10.