Huduma ya kijeshi ya lazima yaani ‘drafting’ ni wakati raia wanatakiwa kisheria kutumikia jeshi, wakati mwingine kwa muda mrefu ikijumuisha kama wanajeshi wa akiba au kwa muda kabla ya kuanza ajira au kuendelea na masomo ya juu.
Wazo hili lilianzia wakati wa Mapinduzi ya Ufaransa na wazo lilikuwa "Kila raia lazima achangie katika kuilinda nchi."
Baadae wazo hili likapata umaarufu wakati wa Vita vya Dunia na wakati wa Vita Baridi.
Lakini baada ya miaka ya 1990 nchi nyingi ziliufuta na kuzingatia zaidi kuunda majeshi la kitaaluma.
Lakini kutoka Ulaya hadi Asia, baadhi ya nchi zimeanza kurudisha tena utaratibu wa kuwalazimisha wananchi kujisajili jeshini.
Basi kwa nini sasa?
Moja, ni kutokana na kuongezeka kwa mvutano wa kimataifa, vita nchini Ukraine, ukosefu wa utulivu wa Mashariki ya Kati na ushindani wa ufahari kati ya mataifa makubwa.
Nchi zinataka majeshi makubwa tena kwa haraka.
Pia siku hizi idadi ya wanaojitolea kujiunga jeshini imepungua, kwani majeshi ya kisasa yanapata tabu kuwaandikisha wanajeshi wapya.
Mwaka huu tu, nchi kama Croatia ambayo ilitangaza kurudisha usajili baada ya kusitisha kwa miaka 17.
Latvia pia inarudisha utaratibu huo, kutokana na kile wanachosema ni vitisho vya kikanda.
Ujerumani inajadili sheria mpya ya 2026 inayotayarisha msingi wa uwezekano wa kurudishwa sera hiyo wakati Uswidi ilianzisha tena katika miaka ya hivi karibuni usajili wa lazima jeshini kwa baadhi ya watu, huku kukiwa na wasiwasi wa usalama.
Faida za huduma jeshini
Takriban mataifa 85 duniani kote bado yanadumisha aina fulani ya huduma ya lazima.
Wale wanaounga mkono mpango huo wanasema unaleta ulinzi imara wa taifa, wanajeshi zaidi, vikosi vikubwa vya akiba na ukakamavu kwa wananchi.
Pia wanaamini huleta nidhamu na ujuzi na hujenga muundo, ushirikiano , ujuzi wa kuishi na muhimu zaidi utayari wa dharura kwani nchi zinaweza kukusanya vikosi haraka katika vita.
Lakini wakosoaji wanasema ni kupoteza uhuru kwani huduma ya kulazimishwa inazuia chaguo la mtu binafsi.
Pia wananukuu athari za kiuchumi kwani vijana wanacheleweshwa kuanza taaluma na ajira zao au kuendeleza elimu hadi watakapomaliza utumishi wao.
Na inafikiriwa kuwa mfumo uliopitwa na wakati kwani vita vya sasa vinategemea teknolojia zaidi, kuliko kuandikishwa kwa wanajeshi wengi.
Kwa hivyo swali kubwa ni, je, kujiandikisha ni kuhusu usalama ... au hofu na maandalizi ya vita vya baadaye?








