| Swahili
AFRIKA
3 dk kusoma
Mackenzie apatikana na hatia ya mauaji ya zaidi ya watoto 190 katika mkasa wa Shakahola Kenya
Mackenzie alishtakiwa kwa kuwaamuru wafuasi wake kufunga pamoja na watoto wao hadi kufa, ili waweze kwenda mbinguni kabla ya mwisho wa dunia.
Mackenzie apatikana na hatia ya mauaji ya zaidi ya watoto 190 katika mkasa wa Shakahola Kenya
Paul Mackenzie bado anakabiliwa na kesi nyingine, ikiwemo mashtaka ya ugaidi. /

Mahakama nchini Kenya, imempata mhubiri Paul Mackenzie na washitakiwa wengine na hatia ya mauaji ya watu 191, wakiwemo watoto 190 na mtu mzima mmoja, katika mkasa wa Shakahola uliotikisa nchi hiyo.

Mahakama hiyo ilitoa uamuzi huo Jumatatu, Oktoba 19, 2026, baada ya kubaini kuwa Mackenzie na wenzake walihusika katika vifo vya wafuasi wa kanisa la Good News International Church, ambao walidaiwa kuelekezwa kufunga hadi kufa kwa imani kwamba wangeingia mbinguni kabla ya mwisho wa dunia.

Mackenzie, ambaye alikamatwa mwaka 2023 baada ya polisi kupokea taarifa kuhusu shughuli za kundi hilo, alikanusha mashtaka ya mauaji. Alidai kuwa hakuwalazimisha kufunga hadi kufa, hata hivyo mahakama ilikataa utetezi huo.

Zaidi ya miili 400 yapatikana Shakahola

Mkasa huo ulianza kufichuka mwaka 2023 baada ya polisi kupata taarifa kuhusu watu waliodaiwa kufariki kwa njaa katika msitu wa Shakahola, ulioko kaunti ya Kilifi, pwani ya Kenya.

Uchunguzi uliofuata uliwawezesha maafisa wa usalama kugundua makaburi ya halaiki na kufukua zaidi ya miili 400.

Miili mingi ilikuwa imeoza , miili 26 pekee iliyokuwa imetambuliwa kufikia wakati wa taarifa zilizotolewa kuhusu kesi hiyo.

Hukumu iliyotolewa Jumatatu ilihusu vifo vya watu 191, wakiwemo watoto 190 na mtu mzima mmoja. Uchunguzi kuhusu vifo vingine vilivyohusishwa na mkasa huo unaendelea.

Jaji Diana Kavedza Mochache, aliyesoma hukumu hiyo kwa zaidi ya saa nane, alieleza kuwa ushahidi uliowasilishwa mahakamani ulionyesha kuwa baadhi ya watoto walitengwa na kunyimwa chakula huku wazazi wao wakishuhudia hali hiyo.

Mackenzie alihudhuria kikao hicho akiwa amevalia shati la polo lenye mistari na suruali nyekundu. Alikaa kimya karibu na mke wake, ambaye pia ni miongoni mwa washitakiwa, wakati hukumu ikisomwa.

Ndugu wa baadhi ya wahanga walifika mahakamani mjini Mombasa kufuatilia uamuzi huo, ambao umekuwa ukisubiriwa kwa hamu kubwa na familia zilizopoteza wapendwa wao.

Rais Ruto awajibika

Kesi hiyo imeibua maswali kuhusu jinsi Mackenzie alivyoendelea na shughuli zake licha ya kuwa tayari alikuwa anafuatiliwa na mamlaka za Kenya miaka kadhaa kabla ya mkasa huo.

Mwaka 2017, polisi walifanya upekuzi katika eneo lake na kuripoti kugundua watoto waliokuwa wakiishi hapo bila kupata elimu.

Baadhi ya wafuasi wake walidai kuwa aliwakataza kuwapeleka watoto wao shuleni na kutafuta matibabu hospitalini walipougua, akidai taasisi hizo zilihusishwa na Shetani.

Mwaka 2019, mamlaka zilifunga kanisa lake, na baadaye alihamishia shughuli zake katika msitu wa Shakahola, kwa mujibu wa taarifa za polisi na vyombo vya habari.

Mkasa huo ulizua wito wa kuimarishwa kwa usimamizi wa makanisa na taasisi nyingine za kidini.

Rais wa Kenya, William Ruto, mwaka 2023 alisema taasisi za serikali zilipaswa kuchukua hatua za kuzuia vifo hivyo na akakubali kuwajibika kama mkuu wa nchi.

 

 

CHANZO:Reuters