| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Familia ya aliyekuwa Rais wa Zambia Lungu yaelekea Mahakama ya Rufani kutokana na mzozo na serikali
Familia inasema Mahakama Kuu ya Pretoria ilikosea kuipa serikali ya Zambia mamlaka ya kusimamia mazishi
Familia ya aliyekuwa Rais wa Zambia Lungu yaelekea Mahakama ya Rufani kutokana na mzozo na serikali
Familia ya Lungu inasema haitaki “serikali ya Zambia iwaambie wapi wanapotakiwa kumzika.” / Reuters

Familia ya aliyekuwa rais wa Zambia Edgar Lungu imeelekea Mahakama ya Rufani ya Afrika Kusini kupinga hukumu ilioruhusu serikali ya Zambia kuurudisha na kuuzika mwili kwa taratibu za mazishi ya kitaifa nchini Zambia.

Familia inasema kuwa Mahakama Kuu ya mjini Pretoria ilikosea kuipa mamlaka hayo serikali ya Zambia kuhusu taratibu za mazishi, ikisisitiza kuwa mjane wa Lungu, Esther Lungu, na watoto wake ndiyo wenye haki kamili ya kuamua wapi na namna gani atazikwa.

Ingawa awali familia hiyo ilijadiliana na serikali ya Zambia kuhusu uwezekano wa mazishi ya kitaifa, wanasema majadiliano yalitibuka baada ya mamlaka kusisitiza kuwa mazishi yataongozwa na Rais wa sasa Hakainde Hichilema.

‘Familia ndiyo yenye maamuzi ya mwisho’

Serikali ya Zambia ilitangaza mwezi Aprili kuwa imeuchukua mwili wa Rais wa zamani Edgar Lungu baada ya mahakama ya Afrika Kusini kuamua kuwa unaweza kusafirishwa.

Lungu alifariki katika hospitali mji mkuu wa Afrika Kusini, Pretoria, Juni 5 mwaka uliopita na hajazikwa mpaka sasa kutokana na mvutano wa majadiliano na kisheria kati ya serikali ya Zambia na familia kuhusu nani mwenye haki ya kusimamia mazishi.

Aliongoza taifa hilo la kusini mwa Afrika kuanzia 2015 hadi 2021.

Mvutano huu wa mahakamani unakuja siku chache kabla ya Zambia kuadhimisha mwaka mmoja tangu kufariki kwa Lungu Juni 5, huku mzozo wa wapi atakapozikwa bado ukiwa haujapata ufumbuzi.

CHANZO:TRT Afrika and agencies