Putin akutana na kiongozi mpya wa Madagascar mjini Moscow

Rais wa Urusi Vladimir Putin amemwambia Kanali Michael Randrianirina kuwa Madagascar ni "mshirika muhimu" barani Afrika.

By
Rais wa Urusi Vladimir Putin, kushoto, na Rais wa Madagascar Michael Randrianirina wakipeana mikono wakati wa mkutano wao mjini Moscow. / AP

Rais wa Urusi Vladimir Putin amekutana na kiongozi mpya wa Madagascar Kanali Michael Randrianirina kwa mazungumzo katika Ikulu ya Moscow siku ya Alhamisi.

Kanali Randrianirina - kiongozi wa muda wa Madagascar tangu aliyekuwa rais kukimbia nchi mwezi Oktoba kufuatia maandamano - amesafiri hadi mjini Moscow wiki kadhaa baada ya Urusi kupeleka vifaa vya kijeshi katika kisiwa hicho.

Putin amemwambia Randrianirina kuwa Madagascar ni "mshirika muhimu" barani Afrika.

"Ningependa kueleza kuwa tuna maeneo mengi ya ushirikiano. Haya ni pamoja kilimo, uchimbaji, nishati, matibabu, huduma ya afya na elimu," kiongozi wa Urusi alisema.

"Tuko tayari kuimarisha ushirikiano wetu katika maeneo ya misaada kwa watu na zaidi," aliongeza.

Putin pia alitoa salamu zake za rambirambi kwa kanali huyo ya jeshi kutokana na kimbunga katika kisiwa hicho, kilichowaua watu wasiopungua 40 mwezi huu.

Ilikuwa moja ya safari za kwanza za kimataifa za rais wa muda Randrianirina. Kabla ya kuondoka Madagascar, aliwaambia waandishi wa habari kuwa amealikwa na Urusi.

Mwezi uliopita, wakufunzi wa jeshi la Urusi lilitembelea Madagascar kuwafunza wenzao kuhusu vifaa vya kijeshi vilivyotolewa na Urusi, ikiwemo ndege zisizokuwa na rubani.

Baada ya ziara ya Moscow, Randrianirina anatarajiwa kuelekea Ufaransa.