Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Misri, Indonesia, Jordan, Pakistan, Qatar, Saudi Arabia, na UAE wamelaani vikali tabia za Waziri wa Israel Itamar Ben-Gvir dhidi ya wanaharakati wa msafara wa flotilla na kuiita "yakushangaza, kudhalilisha na isiyokubalika."
Wanaharakati hao walikuwa wakielekea Gaza na hatimae kuzuiliwa na vikosi vya Israel katika maji ya kimataifa.
Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa Jumapili, mawaziri hao wamesema udhalilishaji wa wazi uliofanywa na Ben-Gvir dhidi ya wanaharakati waliokuwa wanashikiliwa "umekuwa ni udhalilishaji” na "ukiukaji wa wazi" wa Israel dhidi ya haki za binadamu na sheria za kimataifa.
Mawaziri hao pia wamelaani vikali kile walichokiita vitendo haramu vya uchochezi na ukiukaji vilivyofanywa na Ben-Gvir na maafisa wengine wa Israel dhidi ya Wapalestina katika eneo la Palestina linalokaliwa.
Wameonya kwamba vitendo vya uchokozi "vinaongeza chuki na itikadi kali" na kuzuia jitihada za kuleta amani ya kudumu inayojikita katika suluhu ya mataifa mawili.
Taarifa hiyo imetaka Ben-Gvir kuwajibishwa kwa vitendo vyake na kutaka hatua madhubuti zichukuliwe ili kusitisha vitendo hivyo.
Imesisitiza umuhimu wa kulinda haki za binadamu, kuhakikisha hadhi ya binadamu inalindwa, na kufuata sheria za kimataifa katika eneo linalokaliwa la Palestina.
Hatua hii inafuatia kushambaa kwa picha za video zinazomuonesha Ben-Gvir akiwadhihaki wanaharakati waliokuwa wameshikiliwa wakiwa wamepiga magoti huku mikono yao ikiwa imefungwa kwa nyuma.
Msafara wa meli wa flotilla, ulikuwa umebeba watu 428 kutoka nchi 44, uliondoka Marmaris, Uturuki, katika jitihada za kukiuka zuio la Israel la kuingia Gaza, ambalo limekuwepo tangu 2007.


















