Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan, amekutana na Kamishna wa Umoja wa Ulaya anayesimamia Maswala ya Wanachama Wapya , Marta Kos, jijini Ankara, ambapo pande zote zilisisitiza haja ya kuimarisha mazungumzo na ushirikiano katika mazingira ya kijiografia ya kisiasa yanayobadilika kwa kasi.
Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa baada ya mkutano huo uliofanyika siku ya Alhamisi, Fidan na Kos walithibitisha hadhi ya Uturuki kama nchi mgombea wa kujiunga na Umoja wa Ulaya na kusisitiza umuhimu wa kimkakati wa uhusiano wa Uturuki na EU katika kuimarisha utulivu wa kikanda na uimara wa kiuchumi.
Fidan alisisitiza kuwa vikwazo vilivyopo katika uhusiano wa pande mbili vinapaswa kuondolewa bila kuchelewa, akitoa wito wa ushirikiano ndani ya mfumo mpana zaidi, wa kitaasisi na wa pande nyingi.
Pande zote mbili zilipongeza msukumo uliopo hivi karibuni kuhusu suala l na kusisitiza dhamira yao ya kubadilisha mazungumzo kuwa matokeo ya vitendo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hatua iliyopigwa katika mwaka uliopita ni pamoja na kufanyika kwa mikutano mitano ya ngazi ya juu ya mazungumzo, kuendelea kwa msaada wa EU kwa juhudi za Uturuki katika kuwahifadhi wakimbizi chini ya ulinzi wa muda, pamoja na hatua za kurahisisha upatikanaji wa viza za Schengen ya kuingia zaidi ya mara moja kwa raia wa Uturuki.
Muungano wa Forodha, utawala wa sheria na masuala ya kikanda
Pande hizo mbili pia zilikubaliana kuwa maendeleo ya hivi karibuni ya kimataifa na kikanda yamezidi kuonyesha thamani ya kimkakati ya ushirikiano kati ya Uturuki na EU.
Zilisisitiza umuhimu wa kuimarisha uratibu katika usalama na muunganisho wa kikanda, hasa katika maeneo ya Bahari Nyeusi, Caucasus Kusini na Asia ya Kati, kwa kuzingatia sekta za nishati, usafirishaji, masuala ya kidijitali na biashara.
Fidan alibainisha uharaka unaoongezeka wa kusasisha Muungano wa Forodha, akitaja mabadiliko katika mienendo ya biashara ya kimataifa, hali ya kutokuwa na uhakika wa kijiografia ya kisiasa, udhaifu wa minyororo ya usambazaji, pamoja na mabadiliko ya nishati ya kijani na kidijitali.
Pande zote zilikubaliana kuendelea na mawasiliano yenye lengo la kufungua uwezo kamili wa Muungano wa Forodha ili kusaidia ushindani sawa wa masoko na uimara wa uchumi.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa pande zote zilipokea kwa matumaini kurejea taratibu kwa shughuli za Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) nchini Uturuki na kuonyesha nia yao ya kuimarisha ushirikiano katika miradi endelevu na inayoendeshwa na ubunifu.
Kos aliangazia kuwa mazungumzo kuhusu utawala wa sheria na viwango vya kidemokrasia bado ni sehemu muhimu ya uhusiano kati ya Uturuki na EU.
Aidha, Kos aliadhimisha kumbukumbu ya maafa makubwa ya tetemeko la ardhi yaliyotokea Uturuki mwaka 2023, akithibitisha tena mshikamano wa EU, ikiwemo msaada wa dharura na ujenzi upya wenye thamani ya dola bilioni 1.2.
Kwa upande wake, Fidan alisisitiza umuhimu wa kuendeleza mshikamano kati ya Uturuki na EU kwa ajili ya usalama, utulivu na ustawi wa Ulaya.




















