Wanajeshi nchini Afrika Kusini wametibua shughuli za uchimbaji dhahabu haramu katika eneo karibu na mji wa Johannesburg, kulazimisha wachimbaji madini haramu kukimbia na kuacha vifaa vyao.
Polisi pamoja na jeshi walipata vifaa vinavyotumiwa na wachimbaji madini haramu, ikiwemo majenereta na mashine za kuchimba.
Kulikuwa na vyakula na vyombo vya wachimbaji hao kwenye mashimo eneo hilo la Randfontein, karibu kilomita 40 magharibi mwa mji wa Johannesburg.
Operesheni hiyo ni sehemu ya mpango wa serikali kupeleka wanajeshi katika maeneo yenye matukio mengi ya uhalifu, ikiwemo mkoa wa Western Cape, ambao unajumuisha mji wa Cape Town na mkoa ambao ni kitovu cha uchumi wa nchi wa Gauteng.
Magenge ya uhalifu
Huku machimbo ya madini yakiwa yameachwa viungani vya mji wa Johannesburg, uchimbaji madini haramu umeshamiri katika eneo hilo na wachimba madini haramu wanaojulikana kama “zama zama” huingia kwenye machimbo hayo wakitafuta madini ya dhahabu na mengine.
Hairuhusiwi kuchimba madini bila leseni kutoka kwa serikali, na kwa maeneo mengine, mazingira huwa ni hatari zaidi.
Mamlaka zinasema inakadiriwa kuwa kuna wachimbaji madini haramu 30,000 kote Afrika Kusini, wanaofanya kazi katika maeneo 6,000 yaliyoachwa.
Kupotea kwa mapato
Serikali imebaini kuongezeka kwa wachimbaji madini haramu, ambapo wanasema wanapoteza mapato zaidi ya dola bilioni $4 kwa mwaka kwa magenge ya wahalifu.
Biashara hiyo inaaminika kufanywa na wahamiaji kutoka nchi jirani ya Lesotho, Zimbabwe, na Msumbiji, kusababisha hasira miongoni mwa raia wa Afrika Kusini dhidi ya viongozi wa wahalifu na raia wa kigeni wanaoishi miongoni mwao.
Akijibu hoja za wabunge siku ya Alhamisi, Rais Cyril Ramaphosa anasema kupelekwa kwa wanajeshi kutaendelea paoja na hatua zingine kuchukuliwa, kama kuimarisha kikosi cha kukabiliana na magenge na vikosikazi vya kupambana na uchimbaji madini haramu.
















