Mshambulizi wa zamani wa timu ya Nigeria Michael Eneramo amefariki dunia baada ya kuanguka uwanjani wakati wa mechi ya kirafiki siku ya Ijumaa.
Eneramo mwenye umri wa miaka 40 “alionekana kupatwa na mshtuko wa moyo dakika tano baada ya kuanza kwa kipindi cha pili cha mechi hiyo ya kirafiki,” Shirikisho la Soka la Nigeria lilisema, likinukuu taarifa za awali.
Eneramo alicheza kipindi chote cha kwanza huko Ungwan Yelwa, Kaduna, Ijumaa asubuhi.
“Hii inahuzunisha. Sijui niseme nini wakati huu,” Katibu Mkuu wa NFF Mohammed Sanusi alisema.
Eneramo alicheza katika timu ya taifa mara 10 baada ya kukataa kuvaa jezi ya Tunisia, ambapo alipata umaarufu sana wakati akicheza kwenye ligi ya nchini humo na kuwa na wazo la kupata uraia.
Alipewa jina la utani ‘‘Kifaru” na mashabiki wa Espérance Sportive de Tunis, ambao aliwasaidia kushinda “mataji kadhaa,” NFF ilisema. Pia alicheza katika vilabu vya Uturuki Sivasspor, Beşiktaş na Başakşehir miongoni mwa vingine.
Eneramo alicheza mechi yake ya kwanza kwa timu ya taifa dhidi ya Jamaica iliokuwa ya kirafiki Februari 2009, kisha kufunga goli lake la kwanza kimataifa dhidi ya Ireland kwenye mechi iliofuata miezi mitatu baadaye, pia ilikuwa ya kirafiki.











