Wenye magari wamekuwa wakilala kwenye vituo vya mafuta usiku mzima na madereva wa teksi wameshindwa kuendelea na kazi zao huku kwa mara nyingine kukiwa na uhaba mkubwa nchini Malawi.
"Nimelala hapa hapa, na bado nasubiri kuwekewa mafuta," Harry Jim anasema wakati akiwa kwenye foleni ya mafuta. "Kuna uhaba wa mafuta."
Mwendesha bodaboda Paul Christopher, ambaye kawaida hujiingizia kipato kwa kubeba abiria, anasema hajafanya kazi kwa wiki tatu kwa sababu hajafanikiwa kupata petroli.
"Kama mafuta yatapatikana, tutakuwa tunalipa madeni tuliokopa kipindi hiki tukijaribu kujikimu," aliiambia Reuters akiwa nje ya kituo cha mafuta katika mji wa kibiashara wa Malawi, Blantyre.
Tatizo la kila mara
Uhaba wa mafuta limekuwa tatizo la kila mara katika taifa hilo la kusini mwa Afrika kwa miaka kadhaa na ilikuwa suala kuu katika uchaguzi wa mwaka uliopita.
Hali iliimarika kwa muda baada ya Rais Peter Mutharika kushinda uchaguzi na kuongeza bei ya mafuta, lakini ikarudi kuwa mbaya kufuatia kuanza kwa vita vya Iran mwishoni mwa mwezi Februari.
Serikali inasema tatizo hili ni kutokana na uhaba wa fedha za kigeni.
Mutharika ana matumaini kuwa mkopo kutoka kwa Shirika la Fedha la IMF utasaidia kuimarisha hali ya uchumi, lakini hilo bado halijakubaliwa.
























