Mamlaka ya Bandari Kenya, KPA inasema katika kihistoria ya Bandari ya Lamu, Jumapili jioni ilipokea meli kubwa zaidi kuwahi kutia nanga katika Bandari yoyote Afrika Mashariki na Kati.
Meli ya MV Baltimore Express, yenye urefu wa mita 369 kwa ujumla, iliwasili kutoka Bandari ya Salalah ya Oman.
Urefu wa meli hiyo, ni zaidi ya viwanja vitatu vya soka. Kutokana na kina kirefu na urefu wa gati ya mita 400 katika Bandari Lamu, meli hiyo iliweza kutia nanga bila changamoto yoyote.
Meneja Mkuu wa KPA Bandari ya Lamu Kapteni Abdulaziz Mzee aliikaribisha meli hiyo, akibainisha uwezo uliothibitishwa wa bandari kushughulikia meli kubwa zaidi.
"Sisi kupokea meli hii kunainua wasifu wa Lamu kwenye ramani ya kimataifa ya bahari, na kulinganisha na baadhi ya bandari zilizoendelea zaidi duniani kama Singapore, Rotterdam na Hamburg," alisema.
Meli hiyo iliyokuwa ikiendeshwa na kampuni ya meli ya Ujerumani ya Hapag-Lloyd, ikitia nanga Lamu ili kushughulikia marejesho ya shehena iliyokuwa imebeba kemilkali hatari.
Ilisimama ili kuipakia vizuri tena kulingana na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Baharini.
Mnamo Agosti 2025 bandari ya Lamu iliweka rekodi pia kwa kupokea meli kutoka kampuni hiyo hiyo iliyoitwa MV Nagoya Express, meli ya kontena ya mita 335.
Tofauti ya bandari ya Lamu
Kinachoitofautisha Bandari ya Lamu na bandari nyingine za kikanda ni asili ya kina chake kirefu cha mita 17.5.
Bandari nyingine nyingi za Afrika zinahitaji kuchimbwa mara kwa mara ili kuongeza kina ili kubeba meli kubwa na kukaa katika ushindani.
Faida hii ya asili huiwezesha Lamu kushindana na bandari za kisasa zaidi ulimwenguni, na kuziweka sio tu kama lango la kusafirisha mizigo bali pia kama kitovu cha kimkakati chenye uwezo wa kubeba mizigo ya kiwango cha juu sana.
Lamu kufikia sasa imehudumia zaidi ya meli 120 tangu kuanza kwa mwaka huu, huku nyengine nyingi zikitarajiwa kuwasili siku zijazo.
Mamlaka ya Bandari Kenya inasema Ili kukamilisha ukuaji huu KPA inawekeza katika vifaa vya kisasa huku bandari ikitarajiwa kupokea kreni mpya, trekta za mwisho na vifaa vyengine vya kubeba mizigo katika kipindi cha mwaka huu.


















