| Swahili
ULIMWENGU
2 dk kusoma
Watu kadhaa wameuawa katika mapigano kati ya Wahouthi na vikosi vya Serikali nchini Yemen
Mapigano makali yamezuka katika maeneo ya pwani ya Bahari ya Shamu na mkoa wa Taiz, huku vikosi vya serikali vikisema kuwa waasi wa Wahouthi wanajaribu kuitenga mji muhimu wa bandari wa Mokha.
Watu kadhaa wameuawa katika mapigano kati ya Wahouthi na vikosi vya Serikali nchini Yemen
Vikosi vya serikali ya Yemen vinapambana vikali na Wahouthi kusini mwa Hodeida. / / Anadolu Agency

Mapigano kati ya Wahouthi na vikosi vya serikali nchini Yemen yamesababisha vifo vya wapiganaji 81 tangu Alhamisi, kwa mujibu wa maafisa wa kijeshi wa serikali na taarifa kutoka maeneo yanayodhibitiwa na Wahouthi.

Afisa mmoja wa kijeshi katika pwani ya Bahari ya Shamu alisema wanajeshi 24 wa upande wake wameuawa, huku afisa mwingine katika mkoa wa Taiz, akiripoti vifo vya watu 15. Vyanzo vya wizara ya afya katika maeneo yanayodhibitiwa na Wahouthi vilisema kwamba takriban Wahouthi 42 pia wameuawa.

Mapigano hayo yalianza Alhamisi baada ya vikosi vya Wahouthi kuanzisha mashambulizi ya ardhini, yakisaidiwa na mashambulizi ya roketi na ndege zisizo na rubani, katika maeneo ya karibu na pwani ya Bahari ya Shamu na mkoa wa Taiz.

Vyanzo vya kijeshi vya serikali viliiambia Shirika la Gabari la AFP kuwa Wahouthi walikuwa wakijaribu kuutenga mji muhimu wa bandari wa Mokha na maeneo mengine yanayodhibitiwa na serikali. Mji huo umekuwa ukilengwa na mashambulizi kwa wiki kadhaa.

Vyanzo hivyo viliongeza kuwa Wahouthi pia wanajaribu kusonga mbele kuelekea maeneo yanayopakana na Mlango-Bahari wa Bab al-Mandab, njia muhimu ya kimkakati inayounganisha Bahari ya Shamu na Ghuba ya Aden.

Mapigano mapya yaongeza hatari ya kuyumbisha zaidi Yemen

Yemen imekumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa zaidi ya muongo mmoja, kati ya Wahouthi wanaoungwa mkono na Iran na serikali inayoungwa mkono na Saudi Arabia.

Mnamo Julai, Yemen ikawa miongoni mwa nchi zilizoingizwa katika mzozo mpana wa Mashariki ya Kati, baada ya Wahouthi kukiukua makubaliano ya usitishaji mapigano wa mwaka 2022 kati yao na serikali.

Kuibuka tena kwa mapigano kunatishia kuyumbisha hali nchini Yemen, ambako juhudi za awali za kudumisha usitishaji mapigano zilisaidia kupunguza ukubwa na ukali wa mzozo.

Mapigano ya hivi karibuni yamejikita katika maeneo ya karibu na Bahari ya Shamu, njia muhimu sana ya usafirishaji baharini ambayo hupitisha sehemu kubwa ya biashara ya kimataifa.

Hata hivyo, idadi ya vifo iliyotajwa katika taarifa hizi haikuweza kuthibitishwa kwa njia huru.

CHANZO:AFP