| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Uganda yaanza rasmi kampeni ya usafi wa kila mwezi
Wizara ya Uchukuzi nchini humo imeweka tangazo katika mitandao yake ya kijamii ikiwataka wananchi kushiriki ipasavyo katika kile ilichokiita Zoezi la Kitaifa la Usafi.
Uganda yaanza rasmi kampeni ya usafi wa kila mwezi
Serikali imesema zoezi hilo la usafi litafanyika nchi nzima. Picha/Serikali ya Uganda.

Raia wa Uganda wametakiwa kushiriki kikamilifu katika zoezi la usafi lililopangwa kufanyika nchi nzima kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi.

Zoezi hilo limeanza Julai 25, ambayo ni Jumamosi ya mwisho ya mwezi.

Wizara ya Uchukuzi nchini humo imeweka tangazo katika mitandao yake ya kijamii ikiwataka wananchi kushiriki ipasavyo katika kile ilichokiita Zoezi la Kitaifa la Usafi.

Katika kipindi hicho, wananchi wa Uganda wanatarajiwa kufanya usafi katika maeneo yao ya makazi, masoko, shule, vituo vya afya, nyumba za ibada, barabara, mifereji ya maji taka na maeneo mengine ya umma.

Kwa muda wa saa tatu kila mwezi, shughuli zote nchini Uganda zitasimama kupisha zoezi la usafi kufanyika.

Mpango huo ulitangazwa na Waziri Mkuu wa Uganda Robinah Nabbanja ambae amesema kushiriki katika usafi ni "jukumu la kiraia na sio hiyari," na kuonya kuwa wale watakaoshindwa watakabiliwa na "hatua ya utekelezaji."

Hata hivyo, kupitia mitandao ya kijamii, baadhi ya raia wa Uganda wameikosoa kampeni hiyo, na kusema haikutoa muda wa kutosha wa maandalizi.

Mji mkuu wa Kampala pekee unazalisha takriban tani 2,000 hadi 2,500 za taka kila siku, lakini ni nusu pekee zinazokusanywa na kutupwa katika maeneo salama, huku nyengine zikiishia katika mitaro ya maji taka na kuharibu mazingira, kwa mujibu wa mamlaka za jiji.

Msemaji wa Serikali Dennis Patrick Katungi ameiambia AFP kuwa zoezi hilo ni lazima kwa raia wa Uganda kati ya umri wa miaka 18 hadi 65.

"Wale wenye umri zaidi ya miaka 65 na wangependa kushiriki pia wanakaribishwa na wazazi pia wanaruhusiwa kuwashirikisha vijana wao," amesema Katungi.

Harakati zimezuiwa

Kuamikia asubuhi ya leo, sehemu kubwa ya jiji la Kampala ilibaki tupu huku maduka yakiwa yamefungwa huku magari ya polisi yakiweka vizuizi barabara kuzuia magari kupita.

"Magari yote, pikipiki na baiskeli hazitaruhusiwa isipokuwa katika hali ya dharura," imesema polisi nchini Uganda kupitia X.

Ushiriki wa raia wa kigeni

Raia wa kigeni wanaoishi nchini humo pia wanatakiwa kushiriki, ameongeza Nabbanja.

Katika nchi jirani ya Rwanda, utaratibu kama huo umekuwepo tangu mwaka 2007, huku wanaokosa bila sababu ya msingi wakiadhibiwa kwa faini ya hadi Yuro 3.

Burundi pia ilianzisha utaratibu wa lazima wa "kazi za maendeleo ya jamii" mwaka 2006, zinazofanyika kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi.

Utaratibu huo pia uliwahi kuanzishwa nchini Tanzania bara na visiwani Zanzibar, ingawa mpaka sasa utekelezaji wake unasua sua.