Na Göktuğ Çalışkan
Oktoba 13, Emmanuel Macron alimlaki Rais wa Chad Mahamat Idriss Déby Itno katika Ikulu ya Rais ya Élysée. Mawaziri wao wa ulinzi walitia saini makubaliano siku hiyo hiyo ya kuanzisha tena ushirikiano wa kijeshi kati ya mataifa hayo mawili. Wanajeshi wa Ufaransa walikuwa wameondoka Chad miezi ishirini iliopita.
Chini ya miaka miwili, serikali hii hii ilikuwa inawataka wanajeshi wa Ufaransa kuondoka. Kwa kuwa wameondolewa Mali, Burkina Faso na Niger, Ufaransa inahitaji kuwa na ushawishi tena katika kanda hiyo.
Mkutano wa Oktoba unafuatia mikutano kadhaa ya awali. Marais hao wawili walikutana jijini Paris mwishoni mwa mwezi Januari na kisha mjini Nairobi mwezi Mei. Makubaliano yaliyotiwa saini Ikulu ya Élysée ni ishara ya mazungumzo ya miezi kadhaa ya faragha.
Kutoka kwa Oparesheni Épervier na kusitisha ushirikiano
Oparesheni Épervier ilioanzishwa 1986 iliwezesha kuwepo kwa wanajeshi wa Ufaransa nchini Chad kwa zaidi ya miongo mitatu. Wakati Oparesheni Barkhane ilipoanzishwa mwaka 2014, kwa mara nyingine Ufaransa ikaweka makao makuu yake ya kijeshi mjini N’Djamena.
Ukitizama ramani unaweza kuelewa hali ilivyo. Chad iko eneo ambalo jirani wake wa kusini ni Libya na upande wa magharibi ni Sudan, na kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati hadi mpaka wa Niger.
Kuwepo kwa majeshi ya Ufaransa pia kulisaidia kulinda serikali iliyokuwepo madarakani. Mwaka 2008, wakati waasi walipoelekea mjini N’Djamena, Ufaransa ilisaidia kwa kutoa taarifa za intelijensia kwa Rais Idriss Déby. Kulingana na wakosoaji, Ufaransa ilikuwa inaunga mkono uongozi, na uhuru wa nchi ukawa unatiliwa mashaka.
Chad ilisitisha makubaliano ya kijeshi Novemba 28, 2024, jambo lililowashangaza Ufaransa. Wanajeshi 1,000 wa mwisho wa Ufaransa waliondoka Januari 30, 2025. Déby alitaka Chad ifanye maamuzi yake wenyewe kuhusu usalama. Tofauti na nchi za Muungano wa Mataifa ya Sahel (AES), Chad haikusitisha uhusiano wake wa kidiplomasia na kiuchumi na Ufaransa.
Kuondoka kwa wanajeshi wa Ufaransa hakukuwa na athari yoyote kwa tishio lililokuwa linawakabili Chad. Vita vya Sudan vinaendelea eneo la mpaka wa mashariki, ukosefu wa usalama nchini Libya kaskazini, na makundi ya watu wenye silaha eneo la Ziwa Chad vinaendelea kutatiza wanajeshi magharibi mwa nchi.
Mei 4, shambulizi lililosemekana kuwa ni la Boko Haram dhidi ya ngome ya jeshi kwenye kisiwa cha Barka Tolorom liliwaua wanajeshi wa Chad wasiopungua 23 na kuwajeruhi wengine 26. Jeshi lilisema kuwa lilikabiliana na shambulio hilo na kuwaua washambuliaji kadhaa. Kila shambulio la aina hii ni dhihirisho la umuhimu wa nchi hiyo kuwa na taarifa za kijasusi na uwezo wa kukabiliana na mashambulio kwa haraka.
Siyo kila mtu nchini Chad anaunga mkono hatua hiyo. Oktoba 13, chama cha upinzani cha Tchad Uni kilitoa taarifa kikitaka makubaliano hayo na Ufaransa kuheshimu haki za binadamu, misingi ya demokrasia na uwazi na kuhakikisha maslahi ya Chad yanazingatiwa. Serikali ilikuwa imeonesha kuondoka kwa majeshi ya Ufaransa kama hatua ya kusisitiza uhuru wa nchi. Kuhakikisha uhalali wake, itabidi waweke wazi yaliyomo katika makubaliano ya ushirikiano huu wa sasa na kuruhusu taasisi kukagua.
Yaliyotiwa saini Oktoba 13 siyo makubaliano kamili ya ulinzi, na hakuna kambi ya kijeshi ambayo imetengwa kwa ajili ya wanajeshi hao. Hakuna mtu anaeweza kusema kama Ufaransa inajutia kuondoka. Kilicho wazi, ni kuwa, Ufaransa inajaribu kudhibiti tena ilichopoteza, ilhali Déby sasa ana uwezo mkubwa wa kujadiliana kuliko ilivyokuwa awali wakati wanajeshi wa Ufaransa walipokuwa nchini Chad. Wanajeshi wachache na usaidizi wa kijasusi wanaweza kuchukua nafasi ya kambi zilizofungwa mwaka uliopita. Kuna uwezekano gani kwamba uamuzi huu wa sasa utafanywa kwa maslahi ya Chad.
Göktuğ Çalışkan ni mwanafunzi wa uzamifu katika masuala ya uhusiano wa kimataifa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Rabat (UIR). Utafiti wake unaangazia masuala ya Sahel, usalama na uhusiano kati ya Afrika na mataifa ya nje ya kanda.
Kanusho: Maoni ya mwandishi hayaakisi maoni, mitazamo na sera ya uhariri ya TRT Afrika.






















