| Swahili
ULIMWENGU
2 dk kusoma
Jumuiya ya Nchi za Kiarabu yatoa wito wa kulindwa kwa Wapalestina, yapinga kuondolewa kwa lazima
Mawaziri wa mambo ya nje wametoa wito wa utekelezaji kamili wa usitishwaji mapigano Gaza, kuunga mkono mpango wa ujenzi upya na kongamano la kimataifa jijini Cairo
Jumuiya ya Nchi za Kiarabu yatoa wito wa kulindwa kwa Wapalestina, yapinga kuondolewa kwa lazima
Mkutano wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu jijini Cairo, Misri.

Mawaziri wa mambo ya nje wa mataifa ya kiarabu siku ya Jumatatu walitoa wito wa kutaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua mara moja kwa lengo la kuwalinda Wapalestina na kupinga jaribio lolote la kutaka kuwaondoa kwa lazima kutoka katika ardhi yao.

Wito huo ulitolewa baada ya kikao cha mawaziri wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kukutana jijini Cairo, Misri.

Mawaziri hao walitaka jamii ya kimataifa, ikiwemo Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama, kuchukua hatua mara moja ya kuwalinda Wapalestina na mashambulizi ya Israel na vurugu za walowezi wa Israel.

Walitaka kuungwa mkono kwa mpango wa mataifa ya Kiarabu na Kiislamu kisiasa, kifedha na kisheria katika ujenzi upya wa Gaza na kongamano la kimataifa jijini Cairo kuchangisha fedha kwa mpango huo.

Mawaziri hao wanataka utekelezaji kamili wa hatua zote za makubaliano ya kusitisha mapigano ya Gaza yaliyofikiwa katika mkutano wa amani wa 2025 Sharm el-Sheikh, ikiwemo kumalizika kwa mashambulizi ya Israel na ujenzi mpya wa eneo hilo.

Wamepinga moja kwa moja njama yoyote ya kutaka kuwaondoa Wapalestina au kubadilisha muonekano wa maeneo ya Palestina yanayokaliwa, ikiwemo kile Israel inachoeleza kuwa “kuhama kwa hiari.”

Wameonya kuwa kuwaondoa watu kwa lazima itakuwa ni kuangamiza jamii fulani na ukiukwaji mkubwa wa sheria ya kimataifa.

Mawaziri hao pia walishtumu mashambulizi ya Israel huko Gaza, ikiwemo mauaji ya halaiki, njaa,kuzuia watu, uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.

​Jeshi la ​Israel limewaua Wapalestina zaidi ya 73,000 na kuwajeruhi zaidi 174,000 katika vita vibaya zaidi ambavyo vimeharibu sehemu kubwa ya miundombinu ya raia Gaza.

CHANZO:َAA