Uturuki inalenga kuimarisha uwezo wa jeshi lake, ikiwemo la wanamaji, Waziri wa Ulinzi Yasar Guler amesema.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa tamasha la TEKNOFEST Blue Homeland katika Kamandi ya kutengeneza Meli ya Golcuk kaskazini magharibi mwa Uturuki siku ya Alhamisi, Guler anasema nchi hiyo inalenga kuimarisha urithi wake wa muda mrefu katika masuala ya bahari.
“Leo hii, jeshi letu jasiri la wanamaji linaendelea kuwa kikosi thabiti, kinachozuia, na lenye kuheshimiwa katika kulinda haki zetu na maslahi yetu katika maeneo ya bahari yetu, wakiwa na wataalamu waliobobea, miundombinu ya kisasa, meli zilizotengenezwa Uturuki, nyambizi, mifumo isiyo na rubani, na kuendelea kuimarisha uwezo wa teknolojia,” alisema.
“Lengo la Wizara ya Ulinzi ni kuimarisha uwezo wa jeshi letu lenye ujasiri, ikiwemo jeshi la wanamaji, katika viwango vya juu,” Guler aliongeza.
Alisema Uturuki lazima ijitahidi kukumbatia teknolojia zinazoibuka na kuimarisha mafanikio yaliyopatikana katika sekta yake ya nyumbani ya ulinzi kwa kutumia vyema raslimali, kutambua mahitaji sahihi, na kuunga mkono uwezo wa vijana.
Guler alieleza umuhimu wa TEKNOFEST katika kuleta pamoja vijana kwenye sekta ya sayansi na teknolojia, kuhimiza utamaduni wa ubunifu, na kupata watu wanaohitajika kwa ajili ya mpango wa Taifa wa Teknolojia wa Uturuki.
‘Uwezo wa kimkakati wa mustakabali’
Alieleza kuwa watu milioni 1.6 walituma maombi ya kushiriki mashindano ya TEKNOFEST mwaka huu.
Tamasha hilo la Blue Homeland litatoa fursa kwa vijana kuona vyombo muhimu vya Jeshi la Wanamaji la Uturuki, kuanzia meli ya TCG Anadolu hadi manyambizi, alisema.
Guler aliongeza kuwa kila wazo na mradi uliowasilishwa kwenye mashindano hayo kupitia mifumo ya manyambizi ya chini ya maji, roketi za ndani ya maji, na vyombo vya baharini itakuwa ishara ya hatua nyingine ya teknolojia ya baharini kwa ajili ya mustakabali.
“Mradi unaouimarisha leo, mfumo wa kompyuta unaounda, au wazo lenye ubunifu unaloliwasilisha leo linaweza kuwa na uwezo wa kimkakati katika mustakabali ,” aliwaambia washiriki.
Guler alisema wizara hiyo inaunga mkono miradi iliyoanzishwa na vijana na inataka kutengeneza mazingira ambayo yatabadilisha mawazo kuwa teknolojia itakayochangia pakubwa kwa Uturuki.
“Uwezo wa kweli wa Uturuki katika teknolojia utakuwa zaidi kutokana na ari yenu, hamasa, ujasiri, na utashi wa kufikiria zaidi,” alisema.




















