| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Tanzania kuongeza idadi ya ndege ifikapo 2030
Mpango huo, ni sehemu ya juhudi za kuimarisha usafiri wa anga na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa hilo.
Tanzania kuongeza idadi ya ndege ifikapo 2030
Tanzania inalenga kuongeza idadi ya ndege ifikapo mwaka 2030./Picha:Wengine
tokea siku moja

Serikali ya Tanzania imetangaza mpango wa kuongeza ndege nane kwa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), hatua itakayofikisha jumla ya ndege 24 ifikapo mwaka 2030.

Mpango huo, ni sehemu ya juhudi za kuimarisha usafiri wa anga na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa hilo.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Uchukuzi wa Tanzania, David Kihenzile, alipokuwa akizungumza na watumishi wa ATCL katika miji ya Cape Town na Johannesburg, Afrika Kusini.

Kulingana na Kihenzile, shirika hilo lilianza na ndege moja mwaka 2016 na sasa lina ndege 16.

Aidha, katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, serikali ya nchi hiyo,  imeongeza ndege sita kubwa, kwa lengo la muda mfupi kufikia ndege 19 ndani ya mwaka wa fedha 2025/2026, kabla ya kufikia ndege 24 ifikapo mwaka 2030.

Ongezeko hilo la ndege limewezesha kupanuka kwa mtandao wa safari za ndani, ambapo ATCL kwa sasa inahudumia miji ikiwemo Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Kilimanjaro, Arusha, Mbeya, Mtwara, Kigoma, Iringa, Pemba, Unguja, Songea, Mpanda, Tabora na Bukoba.

Pia, ipo mipango ya kuanza safari katika miji ya Sumbawanga, Musoma na Shinyanga hivi karibuni.

Kwenye ngazi ya kimataifa na kikanda, shirika hilo linaendesha safari zake katika miji ya Nairobi, Entebbe, Bujumbura, Lubumbashi, Lusaka, Harare, Johannesburg, Guangzhou (China), Mumbai (India) na Dubai, pamoja na huduma za usafirishaji mizigo zinazochangia kukuza biashara na uchumi wa taifa.

Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, James Bwana, amebainisha kuwa uwepo wa ATCL katika miji ya Johannesburg na Cape Town unachochea ukuaji wa biashara kati ya Tanzania na Afrika Kusini.

CHANZO:TRT Afrika Swahili