| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Kagame awaamuru maafisa waandamizi wa serikali 'kusimama' wakati wa hotuba yake
Video ya Rais wa Rwanda Paul Kagame akiwaagiza baadhi ya maafisa kusimama wakati wa hotuba yake Machi 23, 2026 imesambaa mitandaoni, kusababisha majadiliano kuhusu uhusiano wa uongozi serikalini.
Kagame awaamuru maafisa waandamizi wa serikali 'kusimama' wakati wa hotuba yake
Rais Paul Kagame anasifiwa kwa kuimarisha uchumi wa Rwanda. / Reuters
30 Machi 2026

Video ya Rais wa Rwanda Paul Kagame akiwaagiza baadhi ya maafisa wa serikali kusimama wakati wa hotuba yake Machi 23, 2026 imesambaa mitandaoni.

Kagame ambaye alionekana kuwa na hasira aliwaambia maafisa hao kusimama kwa sababu baadhi yao walikuwa "wanalala" wakati yeye anazungumzia masuala muhimu kuhusu utendakazi wao na maslahi ya wananchi.

Katika hotuba yake, Kagame alieleza makosa kwenye taasisi za umma, kutoajiri wafanyakazi hodari, kutokuwa na vipaumbele mahsusi, matumizi mabaya ya raslimali za umma, na kushindwa kufuatilia utekelezaji wa miradi ya serikali.

Hali hiyo ilijitokeza katika Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi cha Gako, kilichoko Mkoa wa Mashariki mwa nchi.

'Jiuzulu na ufanye mambo mengine kwa uhuru'

Rais Kagame alikuwa katika hafla ya kufunga mkutano uliowaleta pamoja maafisa wa serikali ya taifa na zile za mitaa.

Wale waliokuwepo ni pamoja na mawaziri, magavana wa mikoa, mameya, na wakuu wa mashirika mbalimbali ya serikali.

Akizungumza kwa lugha ya Kinyarwanda, Rais Kagame aliwaambia maafisa: "Nazungumza na baadhi yenu mnalala. Simameni."

Rais aliwaambia maafisa kuwa kama hawataki kuendelea na utumishi wa umma, basi wajiuzulu na "wafanye mambo mengine kwa uhuru."

Kagame aonya kuhusu kujitajirisha binafsi

Kagame aliongeza kuwa baadhi ya maafisa bado "hawamsikilizi" licha ya wao kusimama wima.

Huku kukiwa kimya kote, Kagame alishangaa: "Nyinyi ni watu wa aina gani?"

Katika kumalizia hotuba yake, kiongozi huyo wa nchi alionya maafisa dhidi ya kujitajirisha kwa mgongo wa watu wa Rwanda.

'Ulevi wa madaraka'

Hasa, aliwaambia maafisa wa serikali: "Maslahi ya taifa ni maslahi yenu pia. Hamuwezi tu kuangalia maslahi yenu binafsi na kutarajia kuwa nchi itafaidika, hasa kama unatumia raslimali za nchi kwa maslahi yako binafsi. Hili lazima lifike mwisho."

Pia aliwaonya dhidi ya kulewa madaraka, akisema: "Kuitwa kiongozi pekee, kuitwa 'meya', na hivyo tu, hilo lazima likome."

Alieleza kuhusu ulevi huo wa madaraka na vyeo ni chanzo cha ‘‘ubwirasi", neno la Kinyarwanda linalomaanisha "majivuno" au "ujeuri."

Mkutano huo wa Machi 23, wenye mada "Mwananchi kwanza", uliandaliwa na serikali ya taifa na zile za mitaa kwa lengo la kuimarisha utendakazi wa serikali.

Anasifika kwa kuibadilisha Rwanda

Rais Kagame anasifiwa kwa kubadilisha uchumi wa Rwanda, na wanaompenda wanasifu uongozi wake kama wa "kimkakati na ukakamavu."

Kulingana na ripoti ya Benki ya Dunia 2024, Rwanda inaongoza Kusini mwa Jangwa Sahara kwa ubora wa sera zake za umma na taasisi.

Pia ni sehemu inayoongoza kwa uwekezaji kulingana na sera zake nzuri za kiuchumi.

CHANZO:TRT Afrika