Kampuni za Uturuki zasaini mikataba ya dola bilioni 6.5 kuimarisha mfumo wa ulinzi wa Steel Dome
Mradi huo unajumuisha vipengele 47, vikiwemo rada, makombora, vitambuzi vya kielektroniki vya macho, vituo vya uongozi na udhibiti, pamoja na mifumo ya ulinzi wa anga yenye masafa tofauti.
Makampuni ya ulinzi ya Uturuki yametia saini kandarasi zenye thamani ya dola bilioni 6.5 ili kuimarisha na kuendeleza mfumo wa ulinzi wa anga wa Uturuki, wenye tabaka nyingi na unaotengenzwa nchini humo, Ofisi ya Rais wa Viwanda vya Ulinzi vya Uturuki (SSB) ilisema Jumatano.
Uturuki, mshirika wa NATO ambayo katika miaka ya hivi karibuni imeongeza kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa vifaa vya ulinzi na kupunguza utegemezi kwa wasambazaji wa nje, ilitangaza kwa mara ya kwanza mpango wa kuunda mfumo wa ulinzi wa Steel Dome mwezi Julai 2024.
Mradi huo unajumuisha vipengele 47, vikiwemo rada, makombora, vitambuzi vya kielektroniki, vituo vya uongozi na udhibiti, pamoja na mifumo ya ulinzi wa anga yenye masafa mbalimbali.
Mifumo iliyotengenezwa nchini
Katika taarifa yake, Mwenyekiti wa SSB, Haluk Gorgun, alisema mikataba hiyo inajumuisha mifumo ya kivita na matoleo yake ya kisasa zaidi yatakayobuniwa na Roketsan, na kuongeza kuwa Steel Dome itajengwa kwa kutumia mifumo ya ndani kikamilifu.
Gorgun alisema mikataba hiyo itasaidia kuongeza uwezo wa kuzuia mashambulizi dhidi ya Uturuki, sambamba na kuchangia juhudi za kuongeza masafa na uwezo wa mifumo yake ya kivita.
Wenyeviti wa kampuni za ulinzi Aselsan na Roketsan walisema mikataba hiyo ina "umuhimu wa kimkakati", na wakaongeza kuwa inajumuisha mifumo ya ulinzi wa anga na anga za juu, mifumo ya kupambana na vifaru, pamoja na mifumo mingine ya kimkakati.
Gorgun pia alisema kwamba Uturuki sasa imo miongoni mwa nchi zinazoongoza duniani kwa mauzo ya nje katika tasnia ya ulinzi.