Kubuni miji kwa ajili ya watoto: Muongozo mpya wa maeneo ya umma barani Afrika

Mwongozo mpya wa kimataifa umebuniwa ili kutoa mwelekeo wa vitendo unaolinda na kuimarisha haki ya mtoto ya kucheza kama sehemu ya msingi ya upangaji wa miji.

By Pauline Odhiambo
Miji ya Afrika yanapopanuka, maeneo salama ya umma kwa watoto kucheza, kusonga na kupumua tu yanatoweka. / / Unicef

Kwa Amani mwenye umri wa miaka saba, safari ya kila siku kwenda shule ya msingi katikati ya eneo la viwanda la Mukuru jijini Nairobi ni zoezi la umakini wa hali ya juu. Mkono wake mdogo hushikiliwa kwa nguvu na babu yake wanapopita katika njia nyembamba, wakivuka kwa hofu kila malori ya mizigo yanapopita kwa kasi barabarani karibu nao, huku kukiwa na moshi wa magari uliochanganyikana na ule wa viwanda.

“Ninamwambia atazame malori, si anga,” anasema babu yake Amani, Robert Maina mwenye umri wa miaka 68, akizungumza na TRT Afrika.

“Nilipokuwa mtoto, tulicheza mpira wa miguu pale katika uwanja ule ambapo sasa kuna kiwanda,” anaongeza Robert, akiashiria kipande kidogo cha ardhi kilichosalia. “Sasa mji umekuwa kama mashine, na watoto wetu wanapita tu ndani yake kwa tahadhari kubwa ili wasipate kugongwa.”

Zaidi ya kilomita 4,000 kutoka hapo, mjini Accra, Ghana, simulizi linafanana lakini kwa mtindo tofauti.

Kofi mwenye umri wa miaka kumi humsaidia mama yake kuuza kelewele (ndizi za kukaanga) karibu na maeneo yenye pilikapilika. Eneo lake la kuchezea ni sehemu ya watu kupita ilioko ya kibanda, na vifaa vyake vya kuchezea ni vifuniko vya chupa na mpira.

“Mvua ikinyesha, eneo hili lote hufurika,” mama yake Afia anaeleza, akionyesha mfereji uliojaa taka. “Maji ni machafu na hawezi kucheza. Natamani awe na sehemu safi na kavu ya kuwa mtoto tu, mbali na moshi na kelele. Lakini wapi?”

Viwanja salama vya michezo

Sauti hizi mbili kutoka Nairobi na Accra zinaakisi hali halisi ya maisha ya mijini inayowakumba watu wengi barani Afrika—bara lenye idadi kubwa zaidi ya vijana na linalokua kwa kasi duniani.

Kadri miji ya Afrika inavyopanuka, maeneo salama ya umma kwa ajili ya watoto kucheza, kusogea na hata kupumua yanazidi kutoweka, yakichukuliwa na barabara, ujenzi na makazi yasiyo rasmi.

Hata hivyo, mwongozo mpya wa kimataifa—Mwongozo wa Kuunda Maeneo ya Umma katika Miji kwa Ajili ya Watoto—uliotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO), UNICEF na UN-Habitat, unaeleza kuwa hali hii inaweza kubadilishwa.

Takwimu ni za kutisha. Kiwango cha kimataifa kinaonyesha kuwa ni asilimia 30 tu ya wakazi wa mijini katika nchi za kipato cha chini na cha kati wanaoishi karibu na eneo la wazi la umma. Kwa mamilioni ya watoto wa Afrika, “kucheza” ni shughuli hatarishi inayofanyika kwenye vichochoro vinavyofurika maji, barabara zilizojaa magari au nyumba ndogo zenye chumba kimoja. Uchambuzi wa mwaka 2022 ulibaini kuwa zaidi ya asilimia 60 ya watoto katika miji mikubwa ya Afrika hawana eneo salama la kuchezea ndani ya umbali wa kutembea kwa dakika 10 kutoka nyumbani.

“Upatikanaji wa maeneo ya umma salama na jumuishi una uhusiano wa moja kwa moja na afya, maendeleo, ujifunzaji na mahusiano ya kijamii ya watoto—na ni haki ya mtoto,” anasema Dkt. Etienne Krug wa WHO.

Mwongozo huu mpya unatafsiri haki hiyo kuwa mfumo wa vitendo unaotegemea kanuni sita zinazojulikana kwa kifupi kama ‘SPACES’: Usalama, Mchezo, Upatikanaji, Afya ya Mtoto, Usawa, na Uendelevu.

Kwa wapangaji wa miji na viongozi wa jamii barani Afrika, mwongozo huu unatoa zana zinazolenga changamoto na fursa za kipekee za eneo hili. Unasisitiza kupunguza kasi ya magari na kubuni njia salama za watoto kwenda shule katika miji kama Nairobi, ambako vifo vya watembea kwa miguu ni vingi. Pia unahimiza kuingiza michezo katika maeneo yote ya umma—kubadilisha ua wa zege katika makazi ya Kigali au barabara yenye kivuli huko Lagos kuwa maeneo ya michezo kwa hatua rahisi na za gharama nafuu.

Maeneo rafiki kwa mazingira

Muhimu zaidi, mwongozo unahimiza miji kuwekeza pale hitaji lilipo zaidi. Hii inahusisha kutumia ramani kutambua na kuendeleza maeneo ya kipato cha chini, yenye msongamano mkubwa na makazi yasiyo rasmi—kama Mukuru Nairobi au Ashaiman Accra—ambako mara nyingi hakuna kabisa maeneo ya kijani.

“Mwongozo huu unaonyesha jinsi miji inayomlenga mtoto inaweza kutimiza haki ya kucheza na kuharakisha maendeleo kuelekea maeneo ya umma salama na yanayopatikana kwa wote ifikapo 2030,” anasema Dkt. Nathalie Roebbel, Kiongozi wa Kiufundi wa Afya ya Miji wa WHO.

Kanuni za mwongozo huu zinaendana na mahitaji ya dharura ya Afrika: kuhakikisha hewa safi na kivuli katika miji yenye joto kali, kufufua ardhi isiyotumika, na kuunganisha miundombinu ya kijani na rafiki kwa michezo katika mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Bustani si uwanja wa michezo pekee; ni kinga dhidi ya mafuriko, hupunguza joto mijini, na ni kiunganishi muhimu cha mahusiano ya kijamii. 

Kwa kuwa zaidi ya asilimia 55 ya ukuaji wa miji duniani hadi mwaka 2050 unatarajiwa kutokea Afrika, bara hili lina fursa ya kipekee ya kujenga kwa mtazamo tofauti. Mifereji ya Accra inayofurika mara kwa mara inaweza kubadilishwa kuwa mifumo ya asili ya maji yenye kutoa eneo salama za michezo. Vivyo hivyo, maeneo madogo yasiyotumika katika vitongoji vya Nairobi kama Mukuru yanaweza kugeuzwa kuwa viwanja vya michezo vinavyosimamiwa na jamii. 

Kuanzia mitaa yenye pilikapilika ya Afrika Mashariki hadi jamii changamfu za Afrika Magharibi, wito ni mmoja. Mustakabali wa miji ya Afrika hautaandikwa kwa saruji pekee, bali kwa vicheko vya watoto wanaorejesha haki yao ya kumiliki mji—eneo moja salama, la kijani na jumuishi kwa wakati mmoja.

“Hatuwezi kujenga miji kwa ajili ya benki, magari na majengo, halafu tujiulize kwa nini watoto wetu hawastawi,” anasema Robert Maina jijini Nairobi, huku mjukuu wake Amani akielezea ndoto yake ya kuwa na bustani yenye bembea.

Huko Accra, Afia anaposikia kuhusu mwongozo huu, anakubaliano nalo: “Mahali pa Kofi kucheza si eneo zuri. Eneo la kuchezea ni muhimu kama shule. Hapo ndipo anapojifunza kuishi.”