| Swahili
UTURUKI
4 dk kusoma
Makubaliano ya Makka ni ya ulinzi wa pamoja lakini hayalengi shabaha au adui yeyote: Waziri Fidan
Fidan anasema kuwa muungano huo ni wa kujihami na hauna nia wala mpango wa upanuzi.
Makubaliano ya Makka ni ya ulinzi wa pamoja lakini hayalengi shabaha au adui yeyote: Waziri Fidan
Fidan anasema makubaliano ya ulinzi ya Makka kati ya Uturuki, Pakistan na Saudi Arabia kimsingi ni sawa na NATO. / َAA

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan, amefichua kuwa makubaliano ya ulinzi yaliyotiwa saini kati ya Uturuki, Saudi Arabia na Pakistan mjini Makka yanafanana kimsingi na kipengele cha 5 cha mkataba wa NATO kuhusu ulinzi wa pamoja, lakini yana tofauti muhimu: hayataji adui wa pamoja wala hayalengi nchi yoyote mahususi.

Akizungumza katika mahojiano maalum na shirika la habari la Anadolu siku ya Jumamosi, Fidan alitoa ufafanuzi wa kina zaidi kuhusu makubaliano hayo muhimu ya pande tatu, ambayo aliyataja kuwa hatua ya lazima ya kukabiliana na hali ya ukosefu wa utulivu inayoongezeka katika eneo hilo.

"Makubaliano ya ulinzi ya Makka yanafanana kimsingi na Kipengele cha 5 cha NATO," alisema Fidan, akirejelea kipengele cha ulinzi wa pamoja cha muungano huo ambacho kinachukulia shambulio dhidi ya mwanachama mmoja kama shambulio dhidi ya wanachama wote.

"Makubaliano hayo hayataji tishio lolote la pamoja," alisema Fidan, akiongeza kuwa mataifa hayo matatu yaliingia katika makubaliano hayo kutokana na utambuzi wa pamoja kwamba hali ya ukosefu wa utulivu inayozidi kuongezeka katika eneo hilo ilihitaji mfumo madhubuti wa ulinzi wa pamoja.

Hakuna lengo maalum, hakuna uchokozi

Fidan alisisitiza kuwa muungano huo una lengo la kujilinda na hauna nia wala mpango wa kupanua mipaka yake.

"Hakuna nchi inayolengwa na sisi, mradi tu zisishambulie nchi wanachama," alisema, akionyesha tofauti wazi kati ya kujilinda kwa pamoja na hatua za kijeshi zenye lengo la kushambulia.

Pia alisisitiza kuwa asili ya mataifa hayo matatu yaliyotia saini makubaliano hayo inafanya muungano huo kutokuwa tishio kwa eneo hilo kwa ujumla.

"Uturuki, Saudi Arabia na Pakistan si nchi zenye nia ya kupanua mipaka," alisema Fidan, akionyesha kuwa makubaliano hayo yaliundwa ili kuleta usalama na utulivu — na si kuonyesha nguvu au kutimiza malengo ya kumiliki maeneo mapya.

Kwa nini sasa?

Waziri huyo wa mambo ya nje alisema makubaliano hayo yalitokana na hitaji halisi la kimkakati: kutambua kuwa Mashariki ya Kati na maeneo yanayouzunguka yameingia katika kipindi cha hatari na cha muda mrefu cha ukosefu wa utulivu, hali iliyohitaji hatua za pamoja kutoka kwa mataifa makubwa ya eneo hilo.

Muungano huo wa pande tatu unaziunganisha nchi tatu zenye nguvu kubwa zaidi za kijeshi na kiuchumi katika ulimwengu wa Kiislamu: Uturuki, mwanachama wa NATO mwenye mojawapo ya majeshi makubwa zaidi katika muungano huo; Saudi Arabia, nchi inayotumia fedha nyingi zaidi kwa masuala ya kijeshi katika ulimwengu wa Kiarabu; na Pakistan, taifa lenye silaha za nyuklia na mojawapo ya majeshi makubwa zaidi barani Asia.

Dhamira ya Rais

Fidan pia alisema kuwa dira ya Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, ni kupanua wigo wa Makubaliano ya Pamoja ya Ulinzi ya Makka ili yajumuishe zaidi ya nchi hizo tatu na kuleta nchi zote chini ya mfumo huo ikiwa ni lazima.

Katika ishara muhimu kuhusu upanuzi wa makubaliano hayo hapo baadaye, Fidan alisema anaamini kuwa Misri itajiunga na makubaliano hayo katika awamu yake inayofuata.

Makubaliano ya Makka ni hatua muhimu kuelekea utulivu wa kudumu katika eneo hilo, ambalo kwa muda mrefu limekumbwa na ukosefu wa utulivu tangu kuondoka kwa himaya ya Ottoman, alisema Fidan.

Urusi na Ukraine

Kuhusu vita kati ya Urusi na Ukraine, Fidan alisema kuwa wakati vita vya kuchoshana (vita vya kusuguana) vinapovuka mipaka ya mstari wa mbele wa mapigano, mzozo huo hugeuka kuwa suala la uhai wa taifa.

"Wakati vita vya kuchoshana vinapogeuka kuwa hali ya kuchoshana inayovuka mstari wa mbele, suala la msingi huwa ni je, taifa litaendelea kuwepo? Unatumia njia yoyote ile uliyonayo," alisema.

Kupro

Kuhusu kisiwa cha Kupro, Fidan alisema Uturuki haitambui Utawala wa Wagiriki wa Kupro kama dola huru na kusisitiza kuwa haki za Waturuki wa Kupro lazima ziheshimiwe.

"Hatuitambui upande wa Wagiriki wa Kupro kama dola. Ikiwa hamtambui haki za Waturuki wa Kupro, basi mimi sitambui hadhi yenu ya kuwa dola," alisema Fidan.

"Nyinyi si ile dola iliyoanzishwa mwaka 1960," aliongeza.

Fidan pia alisema kuwa amani na utulivu katika kisiwa cha Kupro vinatokana na uwepo wa askari wa Uturuki kisiwani humo.

Pia alitoa wito wa kuendelezwa kwa hatua ya kimataifa ya kuitenga Israel kisiasa, akisema kuwa hili ni jambo ambalo Israel inaliogopa zaidi.

Israel

Kuhusu Israel, Fidan alikuwa na msimamo usio na shaka, akitoa wito wa kuendelezwa na kuimarishwa kwa hali ya Israel ya kutengwa kisiasa kimataifa, kutokana na mwenendo wake huko Gaza.

"Hali ya Israel ya kutengwa kisiasa kimataifa inapaswa kuendelea bila kukatizwa," alisema, akionyesha kuwa Ankara haina nia ya kulegeza msimamo wake dhidi ya Tel Aviv na itaendelea kushinikiza uwajibikaji katika ngazi ya kimataifa.

CHANZO:َAA