Waziri wa Afya wa Uganda, Chris Baryomunsi, amesema kuwa hakuna maambukizi mapya ya Ebola yaliyoripotiwa.
Waziri huyo alitangaza Jumanne kuwa Uganda sasa haina maambukizi ya Ebola kufuatia mlipuko wa hivi karibuni wa ugonjwa huo wa virusi, uliowaambukiza watu 20 na kusababisha vifo vya watu wawili.
Nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ndiyo kitovu cha mlipuko wa Ebola katika eneo hilo, ambapo idadi ya maambukizi yaliyothibitishwa sasa imefikia zaidi ya 3,000.
"Katika kipindi chote hiki, Wizara ya Afya iliendelea na ufuatiliaji wa kina wa ugonjwa huo kote nchini, na hakuna maambukizi mapya ya Ebola yaliyobainika," amesema Waziri wa Afya Chris Baryomunsi.
Wizara ya Afya imesema Uthibitisho huu unakuja baada ya mgonjwa wa mwisho kutoka hospitali Juni 16, 2026.
Hata hivyo, Shirika la Afya Duniani (WHO) halijatoa ufafanuzi kuhusu tangazo hilo hadi sasa.
Kwa mujibu wa miongozo ya WHO, nchi inaweza kutangazwa kuwa haina Ebola ikiwa hakuna maambukizi mapya yaliyoripotiwa kwa siku 42 mfululizo baada ya mgonjwa wa mwisho kupimwa na kuthibitika kuwa hana virusi, kisha kuruhusiwa kutoka hospitalini.
Hapo awali, Wizara ya Afya ya Uganda ilisema kuwa wagonjwa 17 walipona huku vifo viwili vikirekodiwa. Pia ilieleza kuwa watu watano walioambukizwa walikuwa ndani ya Uganda, huku wengine 15 wamekuja kutoka nje ya nchi.

















