CAF yashusha rungu zito kwa Morocco na Senegal baada ya fujo za katika Fainali ya AFCON 2025
Kupitia Kamati yake ya Nidhamu CAF imetangaza adhabu kali dhidi ya timu za taifa za Morocco na Senegal kufuatia matukio yaliyotokea katika mchezo wa Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 uliyofanyika Januari 18, 2026.
Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF) limeshusha rungu zito na kuzipiga faini kubwa timu za taifa za Morocco na Senegal pamoja na kuwasimamisha wachezaji na makocha wao kwa mechi rasmi zijazo za CAF, kufuatia matukio yaliyoelezwa kuwa ni ukiukwaji wa maadili na kanuni za nidhamu katika Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 iliyofanyika nchini Morocco.
Kupitia Kamati yake ya Nidhamu CAF imetangaza adhabu kali dhidi ya timu za taifa za Morocco na Senegal kufuatia matukio yaliyotokea katika mchezo wa Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 uliofanyika Januari 18, 2026 jijini Rabat nchini Morocco.
Kwa upande wa Senegal, kocha mkuu Pape Bouna Thiaw amesimamishwa mechi tano (5) rasmi za CAF na kutozwa faini ya dola za kimarekani 100,000 kwa mwenendo usio wa kiungwana, huku wachezaji Iliman Ndiaye na Ismaila Sarr wakisimamishwa mechi mbili (2) kila mmoja kwa tabia zisizofaa dhidi ya mwamuzi.
Shirikisho la Soka la Senegal (FSF) pia limepigwa faini ya jumla ya dola 615,000 kwa makosa ya mashabiki wao, wachezaji na benchi la ufundi, na hivyo jumla ya faini kwa Senegal kufikia dola 715,000.
Kwa upande wa Morocco, mchezaji Achraf Hakimi amesimamishwa mechi mbili (2) za CAF, wakati Ismael Saibari akisimamishwa mechi tatu (3) na kutozwa faini ya dola 100,000.
Shirikisho la Soka la Morocco (FRMF) limepigwa faini ya jumla ya dola 315,000 kutokana na mwenendo usiofaa wa vijana waokota mipira, uvamizi wa eneo la VAR na matumizi ya leza kwa mashabiki na kufanya jumla ya faini kwa Morocco kufikia dola 415,000.