Jeshi la Tanzania latangaza nafasi ajira

JWTZ imesisitiza kuwa maombi yote yaandikwe kwa mkono na kuwasilishwa Makao Makuu ya Jeshi Msalato, Dodoma kuanzia Aprili 15 hadi Aprili 28, 2026, yakifuatana na nyaraka muhimu ikiwemo nakala ya kitambulisho cha taifa au namba ya NIDA.

By
Vigezo vingine ni pamoja na kuwa na vyeti halisi vya kuzaliwa na elimu, na kutowahi kuhudumu katika vyombo vya ulinzi na usalama./Picha:@SuluhuSamia

Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limetangaza rasmi nafasi za ajira kwa vijana wa Kitanzania wanaotaka kujiunga na jeshi hilo, likiwahimiza wenye sifa kujitokeza na kufuatilia maelekezo yaliyotolewa.

Kupitia tangazo hilo, JWTZ limeeleza kuwa mchakato wa uandikishaji utafanyika kwa kuzingatia vigezo na taratibu rasmi za jeshi.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Habari na Uhusiano, Luteni Kanali Kevin Byabato, waombaji wanatakiwa kuwa raia wa Tanzania kwa kuzaliwa, kuwa na umri usiozidi miaka 25 kwa wenye elimu ya kidato cha nne na sita, na miaka 28 kwa wahitimu wa elimu ya juu. Aidha, wanapaswa kuwa na afya njema ya mwili na akili, kuwa na tabia njema, pamoja na kutokuwa na rekodi ya makosa ya jinai.

Vigezo vingine ni pamoja na kuwa na vyeti halisi vya kuzaliwa na elimu, na kutowahi kuhudumu katika vyombo vya ulinzi na usalama kama Polisi, Magereza au JKT, isipokuwa kwa waliomaliza mkataba wa mafunzo ya JKT.

JWTZ imesisitiza kuwa maombi yote yaandikwe kwa mkono na kuwasilishwa Makao Makuu ya Jeshi Msalato, Dodoma kuanzia Aprili 15 hadi Aprili 28, 2026, yakifuatana na nyaraka muhimu ikiwemo nakala ya kitambulisho cha taifa au namba ya NIDA, vyeti vya elimu, pamoja na namba ya simu ya mwombaji.