Mbunge wa Jimbo la Biharamulo Magharibi, Ezra Chiwelesa, amesema kuwa suluhisho la tatizo la umeme nchini Tanzania ni Serikali kuruhusu sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika uwekezaji wa nishati ya umeme ili kukuza uchumi wa taifa.
Amehoji iwapo nchi imejiandaa kwa mabadiliko hayo, akibainisha kuwa wawekezaji wengi wanakimbilia kuwekeza nje ya nchi kutokana na changamoto ya mlolongo wa kodi nchini.
Kwa mujibu wake, hali hii inawafanya wazalishaji wa ndani kushindwa kushindana kwa sababu wanabebeshwa mzigo mkubwa wa kodi.
Aidha, amesema kuwa kuna aina mbili za suluhisho katika sekta ya umeme, akisisitiza kuwa haiwezekani kufikia mapinduzi ya viwanda bila kuwa na umeme wa kutosha na wa uhakika.
Ameongeza kuwa si lazima Serikali isimamie kila kitu, ikiwemo uzalishaji wa umeme. Kwa kuwa Tanzania inaendeshwa kwa mfumo wa soko huria, amependekeza sekta binafsi ipewe nafasi ya kuzalisha umeme na kuuza kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Katika sekta ya miundombinu, hususan barabara, amesema pia si lazima Serikali iwe msimamizi mkuu wa ujenzi wake.
Badala yake, ameshauri kutafuta wawekezaji binafsi watakaojenga barabara bora, huku watumiaji wakichangia gharama kupitia mfumo wa kulipia (toll roads).
Pia ameibua changamoto ya ucheleweshaji wa malipo kwa wakandarasi nchini, akisema hali hiyo inakwamisha kasi ya uwekezaji na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.














