Watu wawili wamethibitishwa kufariki kufuatia moto mkubwa uliokumba soko la Gikomba jijini Nairobi mapema Jumapili asubuhi na kuharibu biashara na kuwaacha maelfu ya wafanyabiashara wakihesabu hasara.
Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja alithibitisha kuwa waathiriwa, mwanamume na mwanamke, walikuwa bado hawajatambuliwa rasmi huku timu za dharura zilizofanya kazi kuarifu familia zao.
"Kwa niaba ya wakazi wa Nairobi, ninatuma rambirambi zetu kwa wapendwa wao. Tunasimama pamoja nanyi katika wakati huu wa giza," alisema Sakaja.
Moto wa Jumapili asubuhi uliteketeza sehemu za soko kubwa zaidi la wazi nchini Kenya, na kuharibu bidhaa na miundo mbinu katika sehemu ya kuuzia samaki ya soko.
‘Wazima moto walichelewa’
Watu kadhaa walipata majeraha madogo na kupokea matibabu katika eneo la tukio kutoka kwa wafanyikazi wa ambulensi ya kaunti na Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya.
Wazima moto wanne pia walijeruhiwa wakati wakipambana na moto huo.
Gavana Sakaja alisema maafisa wa kaunti wameanza kutathmini kiwango cha uharibifu na wanashirikisha viongozi kutoka sehemu zote 32 za soko hilo.
Baadhi ya wafanyibiashara walioathiriwa walisimulia kuwa chombo cha kwanza cha zima moto kilichomilikiwa na kaunti kilifika karibu saa 6 baada ya moto huo kuanza, na kusababisha wafanyabiashara waliokuwa na hasira kuwashambulia wahudumu wa kwanza.
Ujenzi mpya
Walihoji zaidi ufanisi wa miundombinu ya zimamoto iliyopo, kwa madai kuwa vifaa vya kukabiliana na moto vilivyo karibu vilikuwa duni wakati wa tukio hilo.
Wakati huo huo Gavana wa Nairobi aliwahakikishia wafanyabiashara kwamba hakuna mtu atakayehamishwa kutoka kwa maeneo yao ya biashara na kuahidi msaada wa kaunti kuwezesha juhudi za ujenzi.
"Tutawaruhusu nyote kujenga upya mahali mlipokuwa hata tunapoendelea kuifanya Gikomba kuwa ya kisasa. Hatutawaacha," gavana alisema.
Soko hilo linasaidia takriban watu 100,000 moja kwa moja kupitia biashara na biashara zinazohusiana, kulingana na takwimu za serikali, na kuifanya kuwa chanzo muhimu cha maisha kwa maelfu ya familia jijini Nairobi.
Viongozi wa wafanyabiashara hapo awali walikadiria kuwa shughuli za biashara huko Gikomba huchangia kati ya 10% na 15% ya pato la kiuchumi la Kaunti ya Nairobi, wakisisitiza umuhimu wake kwa uchumi usio rasmi wa mji mkuu.
















