Iran imedai kuwa baadhi ya nchi za eneo hilo zimeshiriki katika mashambulizi ya Marekani dhidi yake na zimeruhusu maeneo yao kutumiwa na vikosi vilivyotekeleza mashambulizi hayo.
"Nchi ya Marekani inabeba jukumu la uchokozi wa kijeshi dhidi ya Iran ulioanza Februari 28," alisema msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baqaei, wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika Jumatatu.
"Bila shaka, hatuwezi kupuuza ushiriki wa baadhi ya nchi za kanda katika uchokozi huu," alidai.
Baqaei alisema Iran inaendelea kutafuta uhusiano mzuri na nchi jirani na kwamba haina uadui wowote dhidi yao.
"Tumesisitiza mara kwa mara kuwa tunataka kuwa na uhusiano mzuri na nchi za kanda. Kuuna uhusiano mkubwa na maslahi ya pamoja kati ya Iran na nchi za Ghuba ambayo yanaweza kuwa msingi wa kujenga imani na ushirikiano wa pande zote," alisema.
Hata hivyo, msemaji huyo alizituhumu baadhi ya serikali za kanda kwa kuruhusu maeneo yao kutumiwa na majeshi ya Marekani kushambulia Iran.
Msemaji huyo amedai kuwa, "Kwa bahati mbaya, nchi hizi zimeruhusu maeneo yao kutumiwa na wanaofanya uchokozi dhidi ya Iran, jambo ambalo linakwenda kinyume na misingi yote ya sheria za kimataifa na ujirani mwema. Katika baadhi ya matukio, tunajua kuwa zimeshiriki moja kwa moja katika uchokozi huo wa kijeshi dhidi ya Iran."
Nchi za Ghuba zimekuwa zikikanusha mara kwa mara kuhusika katika mashambulizi ya Marekani dhidi ya Iran, huku zikiituhumu Iran kwa kushambulia miundombinu ya kiraia katika mashambulizi yake ndani ya maeneo yao.
"Kama genge la kimafia"
Msemaji huyo pia amesema kuwa kwa sasa Iran haifanyi mazungumzo yoyote na Marekani, na kwamba mazungumzo yoyote yajayo yatategemea kwanza mabadiliko ya tabia ya Marekani. Aidha, amekanusha taarifa kwamba Iran ndiyo ilikuwa imeomba kufanyika kwa mazungumzo na Marekani.
"Hilo haliendani na misingi yetu. Madai kwamba Iran imeomba mazungumzo ni taarifa tu," alisema Baqaei, katika kauli zilizonukuliwa na shirika la habari la Mehr.
Amesema Iran imekuwa ikitumia diplomasia kama chombo cha kulinda maslahi yake ya kitaifa.
"Hatujawahi kusita kutumia njia za kidiplomasia kulinda maslahi yetu ya taifa. Tunaona diplomasia kuwa njia ya kulinda maslahi ya kitaifa ya Iran," alisema.
Ingawa alikiri kuwa kuna wapatanishi wanaoweza kuwa wanapeleka ujumbe kati ya pande hizo mbili, Baqaei alisema: "Kwa sasa, hatufanyi mazungumzo yoyote na upande wa Marekani."
Alipoulizwa kuhusu masharti ya Iran kwa ajili ya kuanza mazungumzo, Baqaei alisema Marekani "lazima kwanza ionyeshe mwenendo wa kuwajibika zaidi."
"Marekani lazima ijifunze jinsi ya kujiendesha kama serikali yenye kuwajibika," alisema, akiituhumu Marekani kwa kujiendesha "kama genge la kimafia" katika kipindi cha mwaka mmoja hadi miwili iliyopita kwa kupuuza sheria za kimataifa.
"Kadiri mwenendo huu unavyoendelea, hatuwezi kutarajia kujenga mazingira chanya yya umma," aliongeza.
Jumapili, msemaji wa jeshi la Iran, Amir Mohammad Akraminia, amesema Marekani imekuwa imesitisha mashambulizi yake katika siku mbili zilizopita na kwamba "operesheni za kujibu mashambulizi" za Iran pia zilikuwa zimesitishwa.
Kwa mujibu wa ripoti ya Axios iliyochapishwa Jumamosi, Rais wa Marekani Donald Trump alikuwa ameagiza jeshi la Marekani lisianzishe mashambulizi mapya dhidi ya Iran, hatua iliyomaliza takriban wiki mbili za mashambulizi ya kila siku.
Mvutano kati ya Marekani na Iran umeongezeka katika wiki za hivi karibuni, huku Marekani ikifanya mashambulizi dhidi ya Iran, na Iran ikijibu kwa kulenga kile ilichodai kuwa ni vituo na vifaa vya kijeshi vya Marekani katika nchi mbalimbali za kanda.
















