Hafla yafanyika Uturuki ya kuwakumbuka wanajeshi waliofariki kwenye ajali ya ndege
Mabaki ya miili ya wanajeshi hao yamepelekwa nyumbani kwao baada ya hafla hiyo.
Hafla ya kuwaaga wanajeshi wa Uturuki waliopoteza maisha kwenye ajali ya hivi karibuni ya ndege ya kijeshi ilifanyika Ijumaa katika Kituo cha Jeshi la Anga cha Murted, jijini Ankara.
Ndege ya Jeshi la Anga la Uturuki aina ya C-130 ilianguka karibu na mpaka wa Azerbaijan na Georgia tarehe 11 Novemba, na kusababisha vifo vya watu wote 20 waliokuwa ndani ya ndege hiyo.
Hafla hiyo ilijumuisha kusimama kimya kwa dakika moja, kusomwa kwa Qur’ani Tukufu na dua kwa ajili ya wanajeshi waliopoteza maisha.
Baada ya kusomwa kwa taarifa za utambulisho wa kila mwanajeshi, majeneza yao yalibebwa na kupelekwa kwenye ndege za kijeshi kwa ajili ya kusafirishwa hadi nyumbani kwao kwa ajili ya kuzikwa.
Miongoni mwa walioudhuria sherehe hiyo ni Spika wa Bunge Numan Kurtulmuş, Waziri wa Ulinzi wa Taifa Yaşar Güler, Waziri wa Familia na Huduma za Jamii Mahinur Özdemir Göktaş, wabunge, makamanda wakuu wa Jeshi la Uturuki, Mkuu wa Mkoa wa Ankara Vasip Şahin, Kamanda wa Jeshi la Anga la Azerbaijan Meja Jenerali Namig Islamzade, Balozi wa Azerbaijan nchini Ankara Reshad Mammadov, pamoja na familia za wanajeshi hao.
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alitoa salamu za rambirambi kwa familia za marehemu, akieleza huzuni yake kubwa kutokana na msiba huo na kuwaombea faraja na nguvu katika kipindi hiki kigumu.